CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Friday, 18 October 2019

VETA yashauriwa kupanua wigo wa ushirikiano na wadau katika kuendeleza ubunifu


Kikao cha Mashauriano kwa ajili ya kuendeleza Ubunifu katika ufundi stadi kilifanyika, tarehe 3 Oktoba 2019 katika chuo cha VETA Kipawa jijini Dar es Salaam huku Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ikishauriwa kupanua mtandao wake wa ushirikiano na taasisi mbalimbali zinazojishughulisha na masuala ya ubunifu ili kusaidia uwezeshaji wa wabunifu katika nyanja mbalimbali. 

Akitoa mada kuhusu, “Fursa za Uwezeshaji wa Ubunifu,” Mkurugenzi wa Mfuko wa Uendelezaji Ubunifu kwa Maendeleo ya Watu (HDIF) nchini, Joseph Manirakiza alisema ufundi stadi unategemewa sana kukidhi mahitaji ya mfumo wa utendaji kazi katika mazingira ya sasa ambapo sekta isiyo rasmi inazidi kupanuka huku ajira kwenye sekta rasmi zikizidi kupungua. 

Alisema ubunifu katika ufundi stadi utasaidia kutatua changamoto nyingi katika jamii ikiwa kutakuwa na mwamko mkubwa miongoni mwa wabunifu na kuweka mikakati mipana ya kuendeleza ubunifu.

Aliishauri VETA kuweka mikakati ya makusudi kuanzisha ushirikikiano na wadau mbalimbali ambao wanaweza kusaidia kifedha au kwa namna nyingine kuendeleza ubunifu wa walimu na wanafunzi wa ufundi stadi. 

“Kutandaa na kubadilisha maarifa kupitia njia za warsha na mikutano kama hii ni muhimu sana katika kuimarisha na kuendeleza mawazo ya ubunifu. Lakini pia mnaweza kuomba ushirikiano na taasisi kama vyuo vikuu na wadau wa maendeleo kwa ajili ya kusaidiana katika maeneo mbalimbali,”  alisema.

Akifafanua zaidi alisema kuwa vyuo vikuu vinafanya utafiti mwingi na hata wanafunzi wake wana mawazo mengi mazuri ya ubunifu, lakini wengi wao wana changamoto katika ujuzi wa kivitendo, hivyo ushirikiano na walimu na wanafunzi wa VETA unaweza kusaidia kutafsiri mawazo hayo katika vitu halisi kwa ufanisi zaidi.

Aliongeza kuwa kuna wadau wengi wa maendeleo ambao sasa wanafadhili sana shughuli za ufundi stadi, ubunifu na ujasiriamali ambao VETA inaweza kuwatumia kwa kuanzisha ushirikiano rasmi katika maeneo mbalimbali ikiwemo ubunifu.

“Hata wale wenye mlengo tofauti katika ufadhili wao, mkienda na hoja nzito bado mnaweza kuwashawishi wakakubali kuwafadhili ikiwa mnachoombea kina manufaa kwa jamii ya Watanzania. Nendeni kwenye balozi na mashirika mbalimbali, waambieni sisi tuna hiki na tunahitaji hiki, wapo wengi wanaoweza kushawishika na kuwasaidieni,”  alisisitiza.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Mhadhiri Mwandamizi kutoka Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela ambaye pia ni mbunifu wa chujio la maji (Nanofilter), Dkt. Askwar Hilonga ambaye alisema VETA ni hazina kubwa ambayo inaweza kutumiwa na walimu na wanafunzi wa vyuo vikuu. 

“Sisi ni wataalam sana kufanya utafiti, kuja na mawazo mazuri ya suluhisho la changamoto mbalimbali, lakini mara nyingi tunaishia kwenye “kupublish paper” (kuchapisha maandiko), ninyi ndio wataalam wa kuunda, mna ujuzi wa kutenda. Kwa hiyo tunaweza kufanya kitu kikubwa tukiwa na ushirikiano na tutatoboa,”  alisema.

Aliishauri VETA kukusaini makubaliano (MoU) na taasisi mbalimbali za elimu ya juu ili kurasimisha ushirikiano katika mambo ya ubunifu. 

Akitoa ushuhuda wa mafanikio yake katika ubunifu alisema, mafanikio katika ubunifu yanaanzia na mbunifu mwenyewe kujitolea kwa dhati na kufanya jitihada kuendeleza ubunifu wake na kwamba ili mbunifu aweze kunufaika vyema na ubunifu wake, suala la kuzingatia changamoto na mahitaji ya jamii ni la kipaumbele kikubwa na kwamba wabunifu wanapaswa kuingiza bidhaa zao sokoni kwa lengo la kupata mrejesho kutoka kwa watumiaji kabla hawajazisambaza zaidi. 

“msibuni vitu ambavyo ni kwa ajili ya kujifurahisha. Angalia jamii inayokuzunguka ina changamoto gani na fikiria unawezaje kutatua changamoto hizo kupitia ubunifu,”  alisema.

Mtaalam wa Mambo ya Haki Miliki, Dkt. Georgies Shemdoe aliwashauri wabunifu kutohangaika sana na kupoteza muda mrefu kuunda vifaa ambavyo vinahitajika katika jamii, kwani  kupitia mtandao wanaweza kuokoa muda kwa kutafuta taarifa kwenye kanzidata za hataza kuhusu vifaa ambavyo vimeruhusiwa kuigwa na kutumika na umma baada ya muda wake wa ulinzi wa hataza kumalizika.

“Taarifa zinaonesha namna ya kutengeneza vifaa hivyo na zingine zina hata michoro. Kwa hiyo badala ya kuumiza kichwa kufikiria na kumaliza mwaka mzima ukihangaika kuunda kitu ambacho tayari kilishavumbuliwa na kinaruhusiwa kuigwa, unaweza kusoma kwenye mtandao na kuunda kitu hicho hata ndani ya mwezi mmoja tu,”  alisema. 

Naye Judith Kadege kutoka COSTECH ambaye alitoa mada kuhusu Haki Miliki na Ulinzi wake aliwahimiza washiriki kujiendeleza kwa kusoma kozi mbalimbali hata kwa njia ya mtandao ili kupanua maarifa katika masuala mbalimbali kuhusu ubunifu. 

Akitoa neno la utangulizi, Meneja Uhusiano wa VETA, Sitta Peter aliwakumbusha washiriki kuwa VETA imejiwekea shabaha katika Mpano wake wa Kimkakati wa miaka Mitano (VCP V, 2018/2019 - 2022/2023) kuhakikisha kuwa walau Mawazo Matano ya Ubunifu yawe yamefikia katika bidhaa au huduma zilizo katika matumizi ifikapo mwaka 2023, hivyo kuwaomba wabunifu kuzingatia mwelekeo huo wanapofanya ubunifu wao.

Washiriki waliipongeza na kuishukuru sana Mamlaka kwa kuandaa mkutano huo na kusema kuwa umekuwa ni wenye manufaa makubwa na umewafumbua na kuwaongezea ufahamu wa mambo mengi ambayo hawakuwa na taarifa au uwezo nayo. 

“Nimejifunza vitu vingi sana na ninashukuru VETA kwa kuandaa forum (mkutano) hii. Ni jambo ambalo halijawahi kufanyika ndani ya VETA. VETA ni kiwanda kikubwa ambacho kinatoa watu ambao wanaenda kufanya kazi katika Tanzania ya Viwanda. VETA inazalisha watekelezaji na watendaji katika viwanda ili viwanda viweze kuendelea kupitia kitengo hiki cha wabunifu, VETA inaenda kutekeleza azimio la Rais la Tanzania ya Viwanda,”  alisema Aneth Mganga, mmoja wa wabunifu walioshiriki mkutano huo.

Washiriki walihitimisha kwa kuweka mapendekezo 15 yanayolenga kwenye kuandaa na kuhuisha sera na miongozo mbalimbali ya uendelezaji ubunifu ndani ya Mamlaka; kuweka miundo na mifumo bora ya usimamizi na uendelezaji ubunifu; kujenga uwezo na kuwezesha wabunifu kupata rasilimali, mashine na nyenzo kwa ajili ya kuendeleza ubunifu wao. 

Mkutano huo uliofanyika kwa siku mbili, tarehe 2 na 3 Oktoba 2019 uliwashirikisha wadau 34 wakiwemo wabunifu wa ufundi stadi kutoka vyuo vya VETA na sekta isiyo rasmi; wataalam wa mambo ya ubunifu na hakimiliki bunifu; wawezeshaji kutoka Taasisi mbalimbali zikiwemo Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH); Wakala wa Usajili na Utoaji Leseni za Biashara (BRELA); Mfuko wa Uendelezaji Ubunifu kwa Maendeleo ya Watu (HDIF) na maafisa kutoka VETA.

Mada zilizowasilishwa na kujadiliwa ni pamoja na, Hali halisi na Mwenendo wa Ubunifu katika Ufundi Stadi; Sera ya Ubunifu ya VETA (2014); Hataza na Haki Miliki Bunifu; Uhawilishaji Teknolojia na Utafutaji wa Taarifa za Hataza katika Mtandao. Nyingine ni Fursa za Ufadhili kwenye Ubunifu; Uandikaji wa Miradi ya Kuomba Fedha; Uandikaji wa Miradi ya Biashara na Jukumu la Chuo cha Walimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC) katika kuendeleza ubunifu kupitia Kituo Atamizi cha Kitaifa cha Ubunifu na Ujasiriamali (VETA NICIE).

No comments:

Post a Comment