CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Wednesday, 4 September 2019

VETA YAANZA MAFUNZO RASMI KWA MAFUNDI WA SIMU ZA MKONONI NCHINI


Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kupitia chuo cha VETA Kipawa imeanza kutoa mafunzo ya Ufundi wa Simu za Mkononi kwa lengo la kuandaa mafundi bora wa simu za mkononi nchini.

Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa mafunzo hayo Agosti 26, 2019, Kaimu Mkuu wa Chuo cha VETA Kipawa Dickson Mkasanga alisema mafunzo hayo yanalenga kuandaa mafundi wa simu za mkononi wenye ujuzi na  weledi watakaofanya kazi zao kwa mujibu wa sheria na kutoa huduma zenye viwango na ubora.

Alisema mafunzo hayo yanatolewa kwa ushirikiano na Mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA) ambapo wahitimu wa kozi hiyo watapatiwa vyeti vitakavyowawezesha kusajiliwa na kupewa leseni ya kufanya kazi za ufundi wa simu za mkononi inayotolewa na TCRA.

Alisema chuo chake pamoja na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) zilishirikishwa na TCRA kubaini uhitaji wa kozi hiyo, umahiri wa mafundi wanaohitajika sokoni na kutengeneza mtaala kwa ushirikiano na wadau mbalimbali na kwamba chuo chake kimejipanga kutoa mafunzo hayo kwa kiwango cha juu.

“Chuo hiki kitatumia rasilimali zake za kisasa na utaalamu wa walimu wake ili kuhakikisha mafunzo haya yanatolewa kwa umahiri na weledi wa hali ya juu”.Alisema

Aliwasihi wanafunzi wa kozi hiyo kuonesha ushirikiano na kufuata taratibu za mafunzo katika hatua zote ili kuwawezesha kupata ujuzi uliokusudiwa na kuwa mahiri katika kutoa huduma za ufundi wa simu za Mkononi.

Naye Mratibu wa kozi hiyo Ricky Sambo alisema mafunzo hayo yamepangwa kutolewa kwa hatua tatu kuanzia hatua ya awali (Basic Mobile Phone Technician) kwa wiki nne, hatua ya kati (Intermediate Mobile Phone Technician ) kwa wiki sita na hatua ya juu(Advanced Nobile Phone Technician ) kwa wiki mbili.

Kwa mujibu wa Sambo, TCRA imetoa ufadhili wa ada kwa wanafunzi 60  kusoma kozi ya awali huku VETA ikitoa waalimu na vifaa vya kuendesha kozi hiyo.

Desemba 2018, Serikali iliagiza kusajiliwa na kupatiwa leseni kwa mafundi wanaotoa huduma za matengenezo ya simu za mkononi ili kuhakikisha huduma wanazozitoa kwa wananchi zinakuwa na viwango stahiki.

1 comment:

  1. Kwa mafundi tuliopo mbeya na momba tunapataje hayo masomo

    ReplyDelete