Wahitimu
wa VETA wasisitizwa kutumia TEHAMA kujiajiri
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (Tehama) Mhandisi Samson Mwela amewataka wahitimu wa VETA
kuitumia vyema taaluma ya Tehama kujiajiri.
Akizungumza katika Mahafali ya Chuo cha VETA
Kipawa leo, Mhandisi Mwela amesema kuwa Serikali imewekeza sana katika
miundombinu ya Tehama ambapo asilimia 94 ya maeneo yanayokaliwa na watu
yamefikiwa na miundombinu ya mawasiliano.
Amesema kuwa vijana waliohitimu katika Chuo hicho
ambacho kinaendesha kozi ya Tehama wana fursa za kujiajiri kutokana na
Mazingira wezeshi ya Serikali katika miundombinu.
Amewataka vijana kuchangamkia fursa hizo hasa kwa
kuzingatia kuwa fursa kwenye sekta hiyo hazihitaji mtaji mkubwa kuweza
kujiajiri na kuwasisitiza kuwa waadilifu katika kazi zao ili kuepuka Uhalifu
kwa kutumia Tehama.
Naye Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabani
nchini Fortunatus Muslim alisema maendeleo ya Tehama duniani yanagusa kila
sekta na kwamba wahitimu hao wanaweza kutumia fursa hiyo kutengeneza mifumo
mbalimbali ya kurahisisha uendeshaji wa shughuli mbalimbali.
Aliwakaribisha wanafunzi kutembelea Jeshi la
Polisi na kujionea mifumo mbalimbali inayotumiwa na jeshi hilo na namna mifumo
hiyo ilivyorahisisha uendeshaji wa shughuli mbalimbali.
Mkuu wa Chuo cha VETA Kipawa Dickson Mkasanga
amesema kuwa Chuo hicho kinaendelea kufanya tafiti na bunifu mbalimbali
zinazolenga kutatua changamoto zinazoikabili jamii pamoja na kuchangia katika
uchumi wa viwanda.
Amesema jumla ya vijana 122 wamehitimu mafunzo
chuoni hapo katika fani za Tehama, Elektroniki na Kompyuta kwa ngazi za Ufundi
Stadi Daraja la pili, Daraja la Tatu, Stashahada pamoja na kozi za muda mfupi
huku chuo hicho kikiwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 250 wa kozi ndefu na
1,800 wa kozi fupi kwa mwaka.
No comments:
Post a Comment