Prof. Ndalichako alitoa rai hiyo
Alhamisi, tarehe 24 Oktoba 2019 alipokuwa akiwahutubia viongozi na wananchi
wilayani Chato baada ya kuweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Ujenzi wa Chuo cha
Ufundi Stadi cha Wilaya ya Chato wenye thamani ya Shilingi za Kitanzania
10,713,316,360.57.
Alitoa mfano wa makampuni ya madini
ambayo yamewekeza katika Kanda ya Ziwa kuwa licha ya kujenga vyuo, yanaweza pia
kusaidia vifaa vya kufundishia na kujifunzia kama mitambo kwa ajili ya maabara
na karakana za vyuo.
“Juhudi kama hizo zimefanyika kupitia
mradi wa IMTT unaoratibiwa na Chuo cha VETA cha Moshi, ambao unawashirikisha
wamiliki wa Migodi ya Geita, Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara. Bila shaka
utaratibu kama huo unawezekana hata kwa Chuo hiki cha Wilaya ya Chato
kitakapokamilika,” alisema.
Sambamba na hilo, Prof. Ndalichako
aliwaomba wananchi na wadau mbalimbali kuhamasisha vijana kujiunga na elimu na
mafunzo ya ufundi stadi, kwani ndio mkombozi mkubwa kwa vijana katika kupata
ajira.
“Mafunzo ya ufundi stadi ni muhimu kwa
kila ngazi, darasa la saba, form four (kidato cha nne), form six (kidato cha
sita) na hata chuo kikuu. Unaweza kujifunza ufundi stadi ili ukusaidie kuingia
kwenye soko la ajira kwa urahisi,” alisema.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati
ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Chato, Dkt. Medard Kalemani aliahidi kuwa
balozi wa ufundi stadi kwa kuhamasisha watu wajiunge na ufundi stadi kila
atakapokuwa na mkutano katika maeneo mbalimbali.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi
Robert Gabriel alisema ana matumaini makubwa kuwa chuo cha VETA Chato
kitasaidia katika ubunifu wa teknolojia za uchimbaji na uchakataji madini
katika mkoa huo ambao umejaliwa utajiri mkubwa wa madini ya dhahabu.
Akitoa maelezo mafupi, Mkurugenzi Mkuu
wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dkt. Pancras Bujulu alisema
Ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Chato ni miongoni mwa miradi
zaidi 40 ya ujenzi wa vyuo vipya vya ufundi stadi na upanuzi wa vyuo vilivyopo
ukilenga kutimiza Lengo la kuongeza usawa wa upatikanaji wa elimu na mafunzo ya
ufundi Stadi nchini.
Alisema, juhudi hizo pia zinasaidia
Vilevile kutimiza shabaha ya kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka wanafunzi
200,000 ya mwaka 2016/2017 hadi 700,000 ifikapo mwaka 2021.
Aliongeza kuwa ujenzi wa chuo hicho
utasaidia kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi
katika mkoa wa Geita ambao kwa takwimu za mwaka huu ulikuwa na vyuo vitatu tu
vya ufundi vya ufundi stadi vikiwa vinamilikiwa na taasisi za dini na binafsi
huku uwezo wa kudahili ukiwa wanafunzi wasiozidi 300 kwa mwaka.
“Kutokana na uhaba wa fursa za mafunzo
ya kuwawezesha kupata ujuzi, vijana wengi wanaishia kutegemea kilimo na uchimbaji
madini mdogo ili kumudu maisha ya kila siku. Kwa kutambua changamoto hiyo, VETA
imeamua kuwekeza katika kujenga vyuo vya ufundi Stadi katika mkoa huu ili ili
kupanua fursa kwa jamii, hasa vijana wa mkoa huu. Licha ya chuo cha Chato,
tunajenga pia chuo cha Ufundi Stadi cha Mkoa katika eneo la eneo la Magogo
mjini Geita,” Alisema
Akieleza kuhusu aina ya mafunzo
yatakayotolewa, Dkt. Bujulu alisema miongoni mwa mambo yaliyozingatiwa ni
pamoja na ukweli kuwa Wilaya ya Chato iko karibu na hifadhi za Taifa za Burigi
Chato na Rubondo, hali itakayosababisha ongezeko la uhitaji wa nguvukazi yenye
ujuzi katika fani za hoteli, huduma ya chakula na utalii kwa ujumla.
“Ili kukidhi haja hii, Chuo cha wilaya
ya Chato kitakuwa na fani ya Mapishi na Uhudumu wa hoteli. Ni matumaini yetu
siku za usoni tutaongeza fani zingine za Ukarimu kama vile uongozaji wa
watalii. Matarajio ni kuwa Mji wa Chato utakua kwa kasi ukipokea wawekezaji
wengi katika sekta ya ukarimu na kukuza uchumi wa wilaya na wanachi kwa
ujumla,” alifafanua zaidi.
Alieleza mambo mengine yaliyozingatiwa
ni kuwa Wilaya ya Chato kuwa na utajiri wa maji ya Ziwa Victoria na hivyo
kuhusisha wananchi wengi katika shughuli za uvuvi, lakini wananchi hawanufaiki
vyema na shughuli hizo kutokana na njia duni za uvuvi na uchakataji
samaki.
“Kwa kutambua hili, chuo cha Chato
kitakuwa na fani ya Uvuvi na Uchakataji wa Mazao ya Samaki ili wahitimu wa fani
hii wakawe chachu ya uongezaji wa mnyororo wa thamani kwa mazao ya uvuvi,”
alisema
Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Elimu
na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Peter Maduki alieleza kuwa licha ya jitihada
zinazofanywa na VETA kuendelea kujenga vyuo katika maeneo mbalimbali nchini,
suala la ubora wa mafunzo linaendelea kuzingatiwa.
Alitaja miongoni mwa jitihada za
kuzingatia ubora wa mafunzo kuwa hivi karibuni Mamlaka imeajiri walimu wapya
400 ambao kwanza walipelekwa kwenye Chuo cha Walimu wa Ufundi Stadi Morogoro
ili kuandaliwa kabla ya kusambazwa kwenye vyuo mbalimbali nchini.
Katika Taarifa yake Fupi kuhusu Mradi,
Kaimu Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Ziwa, Michael Ikongoli alisema Mradi huo
unatekelezwa katika kijiji cha Itale,
Kata ya Muungano, Tarafa ya Buzirayombo, Wilaya ya Chato, Mkoa wa Geita, kwa
gharama za Shilingi za Kitanzania 10,713,316,360.57 ukijumuisha ujenzi wa majengo
27 pamoja na kazi za nje.
Mkandarasi wa ujenzi wa Chuo hicho ni
C. F. Builders Ltd; Msanifu Majengo ni Sky Architects Consultancy; Mkadiriaji
gharama za Ujenzi: Project Group Ltd; Wahandisi Washauri ni RH Engineering
Consultants Ltd na MES Engineering Consultancy Ltd.
Chuo hicho kitakapokamilika kitakuwa
na uwezo wa kudahili wanafunzi 480 kwa mafunzo ya muda mrefu na wanafunzi
wasiopungua 800 kwa mafunzo ya muda mfupi katika kozi za Ufundi Bomba; Ushonaji Nguo; Ufundi
Magari; Uvuvi na Uchakataji wa Samaki; Ukarimu na Huduma ya Vyakula; Umeme na
Uashi.
No comments:
Post a Comment