CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Tuesday 10 December 2019

Maduki Akamilisha Ngwe ya Uenyekiti wa Bodi ya Elimu na Mafunzo ya Ufund Stadi


Aishauri VETA kuzingatia ubora wa mafunzo, uongezaji mapato ya ndani


Bodi ya Taifa ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi imefanya kikao chake leo, tarehe 10 Desemba 2019, na kutumia kikao hicho kumuaga rasmi Mwenyekiti wake, Ndugu Peter Maduki, ambaye muda wake wa Uenyekiti unamalizika rasmi tarehe 16 Desemba mwaka huu. 

Ndg. Maduki aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, tarehe 17 Desemba, 2016, kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi. Kwa mujibu wa sheria, kipindi cha Uenyekiti ni miaka mitatu, ingawa kuna fursa ya kuteuliwa kwa kipindi kingine cha miaka mitatu.

Akitoa shukrani zake kwa Bodi na Menejimenti ya VETA kwa ushirikiano waliompa katika kipindi chake cha Uenyekiti, Ndg. Maduki alitumia fursa hiyo kuishauri Menejimenti ya VETA kuzingatia ubora wa mafunzo ya ufundi stadi wakati ikiendelea na juhudi za kupanua fursa za upatikanaji wa mafunzo hayo.

“Hata mnapokutana na washirika wenu wa maendeleo, zungumzeni nao juu ya hili. Wasiishie kwenye kutusaidia kujenga vyuo tu, waambieni juu ya vifaa na mafunzo kwa walimu na watumishi wetu. Pia tujitahidi kukusanya fedha za ndani na kufanya matumizi bora ya fedha tunazokusanya”
Pia aliishauri VETA kufanya juhudi za kutangaza mafanikio mbalimbali ya VETA na wahitimu wake ili watu waweze kujua na kutambua matokeo ya kazi zake.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Dkt. Pancras Bujulu, alisema kuwa katika kipindi cha miaka minne cha Bodi iliyokuwa chini ya Uenyekiti wa Ndg. Peter Maduki, VETA imepiga hatua katika mambo mengi, yakiwemo utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa vyuo vipya na upanuzi wa vilivyopo; kuenea kwa sifa njema na kuaminika zaidi kwa VETA pamoja na kuongeza udahili wa wanafunzi katika mafunzo ya ufundi stadi. 

“sasa hivi VETA imekuwa brand name (jina maarufu la kibiashara); kila mtu anataka kujihusisha na VETA na tumeaminika sana katika ngazi mbalimbali. Lakini pia umetuunganisha na taasisi mbalimbalii za kitaifa na kimataifa" alisema Dkt. Bujulu.

Naye Mjumbe wa Bodi, Bi. Mary Shuma, kwa niaba ya Wajumbe wote wa Bodi ya VETA, alimshukuru Ndg. Maduki kwa namna yake ya uongozi wa kutumia maneno ya upole katika kutoa maelekezo. Alisema kuwa hiyo ni karama ya kipekee ambayo anapaswa kuidumisha.





No comments:

Post a Comment