Katika
lengo la kuendelea kupanua wigo na fursa za upatikanaji wa elimu na mafunzo ya
ufundi stadi nchini, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)
imetafsiri Mitaala ya fani 24 na Mihtasari 16 katika lugha ya Kiswahili.
Mitaala
na Mihtasari hiyo imekabidhiwa rasmi leo, tarehe 13 Desemba, 2019 kwa Naibu
Katibu Mkuu (E), Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Ave Maria
Semakafu, na inatarajiwa kuanza kutumika kufundishia ufundi stadi katika Vyuo
vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) nchini.
Akizungumza
wakati wa makabidhiano hayo kwenye ofisi za VETA Makao Makuu Jijini Dar es
Salaam, Dkt. Semakafu aliipongeza VETA kwa kukamilisha kazi hiyo na kusema kuwa
ufundishaji kwa Kiswahili kutawawezesha wananchi wengi, kujifunza na kuelewa
vyema mafunzo hayo.
Alisema,
wapo watu wengi walioamua kujifunza ufundi stadi katika mfumo usio rasmi kwa
sababu ya changamoto ya lugha inayotumika kufundishia, kwani wengi wao wana
ugumu kufuatilia vyema mafunzo yanayotolewa kwa lugha ya Kiingereza.
“Tunakwenda
kwenye Uchumi wa Viwanda. Inabidi tukubali kubadilika. Matumizi ya Mitaala ya
Kiswahili iwe hatua ya kwanza. Kuna mengi ya kuboresha. Tufungue milango ili
tupokee mawazo mapya na kuyafanyia kazi. Ufundi Stadi uwe mkombozi kwa jamii
nzima ya Watanzania, hata wanaoendesha shughuli zao za kifundi mitaani,”
alisema Dkt. Semakafu.
Aliishauri
VETA kuchambua na kuona kama kuna haja ya kuwa na kundi la wale wanaotaka
kujifunza kwa Kiingereza kwa lengo la kuendelea na masomo ya juu zaidi, lakini
mafunzo ya jumla yatolewe kwa lugha ya Kiswahili.
Akitoa
taarifa kwa Naibu Katibu Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu
alisema jumla Mitaala 24 na Mihtasari 16 imetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili,
ambapo nakala 240 zimechapishwa kwa kila kitabu, hivyo kufanya jumla ya nakala
za Mitaala na Mihtasari zilizoshachapwa kuwa 9,600.
No comments:
Post a Comment