Mamlaka
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imekutana na wadau wa sekta ya
Hoteli (Ukarimu) na Utalii wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kuweka mikakati ya
kuanza kutoa mafunzo kwa ushirikiano kupitia programu ya Uwanagenzi Pacha (Dual
Apprenticeship training).
Akifungua
warsha hiyo mkoani Mtwara Desemba 17, 2019, Mkuu wa Chuo cha VETA Mtwara Ndugu Joseph
Kibehele amesema utoaji mafunzo kupitia programu hiyo unategemea sana wenye
viwanda, kampuni na hoteli kushiriki kikamilifu.
“Tunawaomba
sana mshiriki katika programu hii ili tuweze kuandaa wafanyakazi wenye viwango
mnavyovihitaji kwenye hoteli zenu.”Alisema
Aliongeza kuwa VETA inatambua umuhimu wa
kushirikiana na viwanda katika kutoa mafunzo kwa kuwa ushirikiano huo
unawezesha kuandaa nguvu kazi mahiri zaidi inayoendana na mahitaji halisi ya
viwanda hasa kwa kuzingatia kuwa sehemu kubwa ya mafunzo hayo yanafanyika sehemu
za kazi.
Mratibu
wa programu hiyo Ndugu. Francis Komba alisema kuwa VETA imeamua kutoa mafunzo
ya Uanagenzi pacha katika sekta hiyo kupitia mfumo huo baada ya Utafiti wa soko
la ajira kufanyika katika mikoa hiyo na kubaini mahitaji makubwa ya wataalamu
wa hoteli na utalii kwa ngazi ya ufundi stadi.
Alisema
mafunzo katika programu hiyo kwa mikoa ya Lindi na Mtwara kwenye fani ya
Ukarimu na Utalii yanatarajiwa kuanza kutolewa mwezi Januari, 2020 kupitia chuo
cha VETA Mtwara.
Kwa
mujibu wa Komba, mafunzo kupitia programu hiyo yanamwezesha kijana kupata ujuzi
wa fani husika akiwa chuoni na sehemu ya kazi, hivyo kumwezesha kwa kiasi
kikubwa kujifunza kwa vitendo na kuendana na mahitaji ya soko la ajira pamoja
na kupata uzoefu na uelewa wa mazingira halisi ya kufanyia kazi.
Meneja
wa Shangani Apartments Ndugu Athumani Akida amesema kuwa mfumo huo wa mafunzo utasaidia
wenye hoteli kupata wafanyakazi bora zaidi kwa kuwa wenye hoteli wanapata fursa
ya kushiriki kuwandaa wakati wa mafunzo. Alisema “Naamini kabisa programu hii
itaondoa lile gap linalojitokeza kati ya sisi waajiri na wanafunzi
wanaozalishwa vyuoni”.
Naye
Afisa Mwandamizi wa hoteli ya BNN Royal Palm Bi. Grace Paul alisema kuwa hoteli
yake iko tayari kushiriki kikamilifu katika kutoa mafunzo hayo na kushauri wadau
wengine kujitokeza kushiriki kutoa mafunzo kupitia programu hiyo yenye faida
kwao.
Mratibu
msaidizi wa programu hiyo Ndugu Fahil Challange alisema kuwa hadi kufika mwaka 2023 VETA inatarajia
kuzalisha wahitimu 15,000 kupitia programu hiyo kutoka 500 wa sasa na kuongeza
fani hadi kufikia tisa kutoka tano zilizoko sasa kutokana na mpango kazi ambao
VETA imeandaa kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja
na Chama cha Waajiri Tanzania ATE.
Mfumo
wa utoaji mafunzo ya Uanagenzi pacha unahusisha kuhudhuria mafunzo ya vitendo
kwenye karakana na darasani (VETA) na kufanya vitendo zaidi katika sehemu za
kazi. Mafunzo hayo ni ya miaka mitatu ambapo kwa kila mwaka mwanagenzi anatumia
wiki 20 VETA na wiki 32 kwa mafunzo ya viwandani.
Mfumo
wa mafunzo ya Uanagenzi pacha ulianzishwa mwaka 2011/12 kwa ushirikiano kati ya
VETA na Hamburg Chamber of Skills Craft ya Ujerumani
ambapo kwa sasa unatekelezwa katika vyuo vinne vya VETA vya Moshi (Ukarimu na
Utalii), Dar es Salaam (Ufundi Umeme na Ufundi Magari), Simanjiro (ufundi
ujenzi) na Manyara (Ufundi wa zana za kilimo).
No comments:
Post a Comment