CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Monday, 2 December 2019

Uzinduzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Ndolage na Uzinduzi wa Mradi wa Ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kagera (Kagera RVTSC)


Tarehe 27 na 28 mwezi huu, VETA iliandaa na kuratibu matukio mawili mkoani Kagera: Uzinduzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Ndolage na Uzinduzi wa Mradi wa Ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kagera (Kagera RVTSC)

Tarehe 27 Novemba 2019, Mhe. Prof. Joyce Lazaro Ndalichako, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia alizindua Chuo cha Ufundi Stadi Ndolage, wilayani Muleba, Kagera. Viongozi wengine wa ngazi za juu waliohudhuria tukio hilo ni pamoja na Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti, Mkuu wa Mkoa wa Kagera; Mhandisi Richard Ruyango, Mkuu wa Wilaya ya Muleba; Mheshimiwa Charles John Mwijage, Mbunge wa Muleba Kaskazini; Emmanuel Shelembi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba; Ndugu Peter Maziku Maduki, Mwenyekiti wa Bodi ya VETA Taifa; Mama Rifai Mkumba, Mkurugenzi wa Bodi Kuu ya VETA na Dkt. Pancras Bujulu, Mkurugenzi Mkuu wa VETA.

Ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Ndolage uliasisiwa na wananchi wa Kijiji cha Bushagara kwa Kushirikiana na Wadau mbalimbali, akiwemo Mbunge wa Jimbo la Muleba Kaskazini Mhe. Charles Mwijage. Madhumuni ya awali yalikuwa kuanzisha Shule ya Sekondari, lakini baadaye walibadili mawazo na kuamua kiwe chuo cha Ufundi Stadi.

Serikali kupitia VETA iliwasaidia wananchi kukamilisha ujenzi huo. Ujenzi huo ulifanywa na kikosi cha Ujenzi cha Chuo cha VETA Kagera kwa kutumia mfumo wa nguvukazi na uwezo wa ndani (yaani Force account) chini ya Mhandisi Mshauri kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Muleba.

Ujenzi wa Mradi huo ulitengewa kiasi cha fedha cha Tshs 281,575,270.6. Fedha zilizotumika ni Sh. 260,268,912.24 na fedha zilizobaki, Sh. Shilingi 21,600,000 zitatumika kuendeshea mafunzo.

Chuo kina uwezo wa kudahili wanafunzi 80 (yaani wanafunzi 20 kwa kila fani) kwa mwaka, kwa masomo ya muda mrefu (yaani Miaka 2) na Wanafunzi 300 kwa kozi za muda mfupi (Short course). Chuo kitaanza kutoa Mafunzo mwezi Januari 2020, fani za fani za Uashi, Ushonaji, Uchomeleaji na Uundaji Vyuma, Uhazili na Computer. Pia mafunzo ya muda mfupi yakiwemo Udereva, Ufumaji, Mapambo na zingine kutegemea na mahitaji yatakayojitokeza.

Tarehe 28 Novemba 2019, Mhe. Prof. Joyce Lazaro Ndalichako, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Mhe. Wang Ke, Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania walizindua Mradi wa Ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kagera (Kagera RVTSC) unaojengwa kwa ufadhili wa Serikali ya China. Viongozi wengine wa ngazi za juu waliohudhuria uzinduzi huo ni pamoja na Mheshimiwa Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti, Mkuu wa Mkoa wa Kagera;  Mheshimiwa Deodatus Lukas Kinawiro, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba; Mheshimiwa Costansia Nyamwiza Buhiye, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (uliyemwakilisha Dkt. Bashiru Ally, Katibu Mkuu wa CCM); Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini; Ndugu Peter Maziku Maduki, Mwenyekiti wa Bodi ya VETA Taifa; Mama Rifai Mkumba, Mkurugenzi wa Bodi Kuu ya VETA na Dkt. Pancras Bujulu, Mkurugenzi Mkuu wa VETA.

Mradi wa ujenzi wa Kagera RVTSC wenye thamani ya Sh. Bilioni 22.04 unatekelezwa katika eneo la Burugo kata ya Nyakato, Wilaya ya Bukoba na Mkandarasi ni Kampuni ya Kichina ya Shanxi Construction Investment Group Company Ltd. na kusimamiwa kwa pamoja na Kampuni za Kichina za China Qiuyan Engineering Corporation na Xian Sifang Construction Supervison Co. Ltd. Eneo la ujenzi wa Chuo hicho cha lina ukubwa wa hekta 40.58.
Mradi huu unategemea kukamilika baada ya miezi 18, na utajumlisha shughuli za ujenzi, samani, mitambo, zana na vifaa vya kujifunzia.

Majengo yatakayojengwa ni pamoja na Madarasa – 14; Ofisi za Walimu – vyumba 9; Karakana – Majengo 3 yenye karakana 8; Lecture theaters – 2; Jengo la Utawala – vyumba 18; Nyumba za Walimu (Mwl. Mkuu 1, Wafanyakazi familia 2); Mabweni ya Wanachuo – Mawili (200 wa kiume, 120 wa kike); Jiko na Bwalo la Chakula; Matanki ya maji; Vyoo – majengo 2; Maabara za Kompyuta – 1; Bohari (Stoo) – 1 na Uzio.

Karakana zitakazojengwa ni pamoja na Umeme wa majumbani na viwandani; Uchomeleaji na uungaji vyuma; Ufundi magari; Mitambo; Ufundi bomba; Useremala; Uashi; Ufundi rangi na Uchorongaji wa ardhi.

Chuo kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 800 wa kozi za muda mrefu na zaidi ya 2,000 wa kozi za muda mfupi. Hata hivyo, Chuo kitakuwa na mabweni kwa wanafunzi 200 wa kiume na 120 wa kike.


No comments:

Post a Comment