Mkuu wa
Wilaya ya Arumeru Mhe. Jerry Muro amewataka wahitimu wa Chuo cha VETA cha Mafunzo
ya Hoteli na Utalii kuchangamkia fursa zinazotokana na kukua kwa sekta ya
utalii nchini.
Mhe. Muro
aliyasema hayo katika Mahafali ya saba ya Chuo hicho yaliyofanyika Novemba 29,
2019 Njiro, jijini Arusha ambapo jumla ya vijana 89 walihitimu katika ngazi za
Astashahada na Stashahada katika kozi za hoteli na Utalii.
Alisema sekta
ya Utalii inazidi kukua siku hadi siku kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa
na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli
hasa katika kuboresha miundombinu kama vile ujenzi wa viwanja vya ndege na
ununuzi wa ndege mpya pamoja na ujenzi wa barabara.
“Utalii
unakua na kuongezeka kwa kasi kubwa sana ambapo zamani tulitegemea zaidi watalii
kutoka nchi za Ulaya na Marekani lakini
kwa sasa tunashuhudia watalii kutoka nchi za Asia kama vile China na India
wakija nchini kwa wingi ambapo mahitaji ya huduma katika sekta hiyo yanazidi
kuvutia wawekezaji wakubwa na wadogo… hizi ni fursa kwa wahitimu wetu hivyo
zichangamkieni” Alisema
Aliishauri
VETA kuongeza udahili katika kozi za ukarimu na utalii ili kuzalisha nguvukazi
ya kutosha kuhudumia sekta hiyo inayokuwa kwa kasi na kuandaa mafunzo ya muda
mfupi kwa madereva na waongoza watalii ambao hawajapitia mafunzo maalum ili
waweze kuendesha shughuli zao kwa viwango vinavyokubalika kimataifa.
Awali, Mkuu
wa Chuo cha VETA Njiro Christopher Ayo alisema kuwacasilimia tisini na nne
(94%) ya wahitimu hao wameshaajiriwa na kuongeza kuwa takwimu hizo ni ushahidi
wa ubora wa mafunzo yanayotolewa na chuo hicho na juhudi za kuunga mkono dira
ya nchi ya kujenga uchumi wa viwanda.
Alisema chuo hicho chenye
usajili na ithibati ya Baraza la Elimu ya Ufundi yaani NACTE kimekua kikitoa
mafunzo katika kozi za mapokezi na huduma za malazi (Rooms Division), huduma na
mauzo ya chakula na vinywaji (Food and Beverage Services and Sales) na sanaa ya uandaaji na mapishi (Culinary Art) katika
ngazi ya Astashahada na Stashahada.
Aidha Chuo hicho kimeanza
rasmi kutoa mafunzo ya muda mrefu katika kozi za uongazaji watalii (Tour Guide)
kwa ngazi ya Astashahada na usimamizi wa uendeshaji shughuli za watalii (Travel
and Tour Operations) kwa ngazi ya Stashahada ambazo zitaendeshwa kwa muda wa
miaka miwili.
Ayo alitaja baadhi ya mipango ya chuo hicho kuwa ni
pamoja na kuongeza udahili hadi kufika wanachuo mia tano (500) kwa mwaka kutoka
mia tatu (300) wa sasa, kuongeza ushirikiano na vyuo na taasisi mbalimbali
ndani na nje ya nchi zinazotoa mafunzo ya hoteli na utalii na kuanzisha masomo
kwa njia ya mtandao (E-learning) hasa kwa wahitaji walio mbali na chuo wanaotaka
kujiendeleza.
Ayo alisema chuo kinatoa
mafunzo ya muda mfupi katika fani mbalimbali kama Upambaji, Usafi wa majengo na
maeneo ya wazi, Upishi, Huduma ya uuzaji vinywaji, uandaaji wa keki na mafunzo
ya uongozaji watalii.
No comments:
Post a Comment