Kwa kuzingatia mahitaji
ya ujuzi kwenye sekta za Kilimo na Mifugo, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi Stadi (VETA) iko katika hatua za juu za majadiliano na Chuo cha Ufundi
Stadi wa Kilimo Henan cha nchini China kwa lengo la kuanzisha chuo maalum cha ufundi
stadi kitakachobobea katika utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi katika fani za
Kilimo na Mifugo.
Ujumbe wa timu ya
viongozi na wataalam 9 kutoka Chuo cha Henan, ukiongozwa na Makamu wa Rais wa
Chuo hicho, Prof. Wu Guozhao, umekuwepo nchini kwa siku mbili, tarehe 18 na 19
Desemba 2019 kwa ajili ya kutembelea vyuo vya VETA na kufanya mazungumzo ya
awali na Menejimenti ya VETA juu ya mpango huo. Timu hiyo ilitembelea na
kujionea mazingira na hali halisi ya utoaji mafunzo katika vyuo vya VETA
Kihonda kinachotoa mafunzo katika Fani ya Ufundi wa Zana za Kilimo na Chuo cha
TEHAMA cha VETA Kipawa. Ikiwa Morogoro,
timu hiyo ilipata pia fursa ya kutembelea Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
(SUA) kwa lengo la kupanua zaidi ufahamu wa mafunzo ya kilimo yanavyotolewa
nchini.
Akizungumzia wakati wa
majadiliano na ujumbe huo, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu amesema
ana imani kubwa kuwa mpango wa ujenzi wa chuo hicho utawavutia wengi na unagusa
sekta ya kipaumbele kikubwa katika jamii.
Alisema asilimia kubwa
ya Watanzania wanaishi kwa kutegemea kilimo na hata wafanyakazi na
wafanyabiashara wengi nchini pia wanapenda kujishughulisha na kilimo.
“Mathalani, kwa miaka
mingi watu wengi wanaulizia mafunzo ya Kilimo cha Mazao ya Bustani, Usindikaji
wa Mazao ya Chakula na hata Kilimo cha Mazao ya Nafaka. Kwa ujumla naona kuna
mahitaji mengi ya ujuzi katika eneo la kilimo. Bila shaka mpango huu utaungwa
mkono na Serikali yetu tukufu ya awamu ya tano,” alisema Dkt. Bujulu.
Alisema VETA ina nia ya
kuimarisha mafunzo katika sekta ya Kilimo na Mifugo na miongoni mwa malengo ni
kuwa na chuo mahsusi kitakachobobea na kuwa kituo bora cha mfano katika mafunzo
ya ufundi stadi kwenye sekta za Kilimo na Mifugo.
Katika vyuo
vinavyomilikiwa na VETA, mafunzo ya muda mrefu ya ufundi stadi yanayogusa sekta
ya kilimo hutolewa katika fani za Ufundi wa Zana za Kilimo (VETA Kihonda, VETA
Manyara, VETA Arusha-Oljoro, VETA Mpanda na VETA Dakawa); Ufugaji (VETA
Singida); Teknolojia ya Usindikaji wa Nyama (VETA Dodoma). Vilevile VETA huendesha
kozi za muda mfupi ambazo ni za kati ya miezi miwili hadi sita kupitia programu
yake ya Uboreshaji Ujuzi kwa Wajasiriamali kwenye Sekta Isiyo Rasmi (INTEP)
ukihusisha mafunzo mbaimbali kama Kilimo cha Uyoga, Ufugaji wa Samaki,
Utengenezaji Mvinyo, Usindikaji wa Mboga na Matunda, Usindikaji wa Samaki na
Usindikaji wa Asali.
Kwa upande wake Makamu
wa Rais wa Chuo cha Henan, Wu Guozhao amesema ni vyema kuweka mpango maalum wa
utekelezaji wa wazo hilo la kujenga chuo kwa ushirikiano na kuhakikisha kuwa
pande mbili zinauridhia kabla ya kuanza kuutekeleza hatua kwa hatua.
“Hata sisi tunahitaji
ridhaa ya Serikali yetu. Chuo chetu kinaendeshwa kwa fedha za serikali,
tunaweza kupata msaada wa serikali kwa kiwango fulani. VETA nanyi mnapaswa
kuzungumza na serikali ili kupata ridhaa yake na kuomba ufadhili kwa ajili ya
ujenzi na uendeshaji wa chuo hicho,” amesema Guozhao.
Ameongeza chuo cha
Henan kitatumia uzoefu wake katika mafunzo mbalimbali kwenye eneo la Kilimo na
kushirikiana na VETA katika kubuni na kuanzisha
kozi ambazo zitawiana na mahitaji ya Watanzania.
Mazungumzo hayo
yamehitimishwa kwa makubaliano ya VETA kuandaa Andiko la Mradi wa Chuo cha
Ufundi Stadi wa Kilimo na kuainisha na kuliwasilisha kwa Serikali ya Tanzania
ili kupata ridhaa yake, kabla ya hatua zingine za majadiliano ya utekelezaji
kuendelea.
Miongoni mwa mambo
ambayo Andiko hilo linapaswa kuainisha ni muundo utekelezaji wa majukumu na
ushiriki wa pande zote mbili (yaani Chuo cha Henan na VETA) katika gharama za
ujenzi; ununuzi wa vifaa; uandaaji wa mitaala; muundo wa fani; utungaji
mitihani na utoaji vyeti na usimamizi wa chuo. Vilevile, imekubalika kuwa
Andiko linatakiwa kupendekeza mahali pa kujenga chuo kwa kuzingatia vigezo
mbalimbali pamoja na kuainisha kozi zitakazofundishwa na utaratibu wa kuanza
kwa kozi hizo hatua kwa hatua.
Tayari VETA na Henan
zilishasaini Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) katika maeneo mbalimbali ya
utoaji mafunzo na uendelezaji ujuzi tangu Desemba mwaka jana na hatua
mbalimbali za utekelezaji wa MoU hiyo zimeshafanyika ikiwa ni pamoja na kutembeleana
na kubadilishana uzoefu.
Miongoni mwa matunda ya
hivi karibuni ya makubaliano ufadhili na Chuo cha Henan kwa walimu 10 kutoka
vyuo mbalimbali vya ufundi stadi kujiunga na mafunzo ya miaka mitatu katika
fani mbalimbali za kilimo katika chuo hicho nchini China. Walimu hao wataondoka
mapema Februari 2020 kwa ajili ya kwenda kuanza masomo.
Chuo cha Henan cha
Ufundi Stadi wa Kilimo (Henan Vocational College of Agriculture) kilianzishwa
mwaka 1952. Chuo hicho kilichopo katika jimbo la Henan kinachomilikiwa na
serikali ya China ni chuo cha mfano katika utoaji wa elimu ya ufundi stadi
katika fani mbalimbali za kilimo ikiwa ni pamoja na kilimo cha bustani na
mbogamboga, ufugaji na usindikaji wa chakula.
No comments:
Post a Comment