Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)
imesaini makubaliano na Wizara ya Kilimo kwa ajili ya kutekeleza mradi wa
Kudhibiti Sumukuvu nchini Tanzania, kwa Kiingereza "Tanzania Initiatives
for Preventing Aflatoxin Contamination (TANIPAC)".
Makubaliano hayo yametiwa saini leo kati ya Mkurugenzi
Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mhandisi
Mathew Mtigumwe, aliyewakilishwa kwenye hafla hiyo na Mkurugenzi wa Utawala na
Rasilimali Watu wa Wizara ya Kilimo, Bi. Hilda Kinanga.
Jukumu la VETA katika mradi wa TANIPAC ni kutoa
mafunzo kwa vijana 400 katika kutayarisha vihenge vya chuma (metal silos) kwa
ajili ya kuhifadhia mazao.
Mradi huo utakaotekelezwa kwa miaka mitano, kuanzia
2019 hadi 2023 unalenga kushughulikia changamoto ya usalama wa chakula,
hususani Sumukuvu, katika mnyororo wa thamani wa mazao ya karanga na
mahindi.
Akizungumza baada ya kutia saini makubaliano hayo,
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Bujulu, amesema VETA imelipokea jukumu hilo kama
fursa ya kipekee, kwani ingawa imekuwa ikitoa mafunzo kwenye fani mbalimbali za
kilimo, ni mara ya kwanza kupewa jukumu maalum kwa ajili ya mafunzo ya
utengenezaji wa vihenge (silos).
_“Tuko tayari kutoa mafunzo hayo kwa hao vijana 400
waliolengwa na mradi huu ambao watakuwa chachu katika kusambaza teknolojia hiyo
nchini. Lakini hatutaishia hapo tu, bali tutatoa kwa Watanzania wengine
watakaohitaji mafunzo hayo ili kusaidia kulinda afya za walaji na kuongeza tija
kwenye kilimo,”_ Dkt. Bujulu amefafanua zaidi.
Kwa upande wake Bi. Kinanga ameishukuru VETA kwa
kukubali ushirikiano huo na kueleza kuwa ana matumaini kuwa ushirikiano huo
utaweza kuleta matokeo yaliyotarajiwa.
No comments:
Post a Comment