CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Tuesday 4 February 2020

VETA yaingia makubaliano na MUST kushirikiana kuboresha ufundishaji wa ufundi nchini


Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imesaini makubaliano ya ushirikiano na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) kuboresha utoaji wa mafunzo ya ufundi na kuzalisha mafundi bora nchini.

Akizungumza wakati wa tukio la utiaji saini makubaliano hayo Februari 4, 2020 katika ofisi za VETA Makao Makuu Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu amesema kuwa makubaliano hayo yanalenga kushirikiana na kubadilishana uzoefu kwenye ufundishaji, utafiti, ushauri elekezi, ubunifu, teknolojia na utoaji huduma.

Dkt. Bujulu amesema VETA inalenga kupeleka walimu wake kupata mafunzo ya elimu ya juu kwa ngazi za Stashahada, Shahada na nyingine katika chuo cha MUST kwa ajili ya kuboresha uwezo wao katika ufundishaji na utafiti.

“kwetu ni heshima kushirikiana na chuo kikuu cha MUST kwa kuwa kuna maeneo mengi tunayorandana na hivyo kupitia ushirikiano huu sisi tunayo mengi ya kujifunza kwao na wao wanayo ya kujifunza kwetu pia”. Alisema

Dkt. Bujulu ameongeza kuwa VETA na MUST watashirikiana katika kufanikisha shughuli mbalimbali za ufundi na kuboresha mafunzo kwenye fani mbalimbali zinazotolewa kwa wanafunzi wa taasisi hizo.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo cha MUST Prof. Aloys Mvuma amesema MUST imekuwa ikishirikiana na VETA kwenye maeneo mengi kwa muda mrefu na kwamba wameona umuhimu wa kuweka rasmi ushirikiano huo.


“Tunaamini kupitia ushirikiano huu tutaweza kubadilishana wataalamu na kujengeana uwezo katika utoaji  mafunzo na zaidi mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa pande zote mbili kupitia karakana na maabara zilizopo kwenye vyuo”; amesema Prof. Mvuma.

Prof. Mvuma ameongeza kuwa ushirikiano huo pia unalenga kuendeleza ubunifu wa wanafunzi wa chuo Kikuu cha MUST na vyuo vya VETA hadi hatua ya kubiasharishwa.


2 comments: