Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, amezindua sare
mpya za madereva na makondakta wa daladala Jijini Dar es Salaam ambapo Mamlaka
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imepewa tena zabuni ya kuendelea
kushona sare hizo.
Kwa mara ya kwanza VETA ilipewa zabuni ya
kushona sare hizo mwaka 1998.
Uzinduzi
wa sare mpya umetokana na mahitaji na mawazo ya uboreshaji wa sare hizo
yaliyotolewa na Chama cha Wamiliki wa Daladala (DARCOBOA) na Umoja wa
Wasafirishaji Abiria Jijini Dar es Salaam (UWADAR).
Sare
hizo zinajumuisha kaunda suti za rangi ya zambarau na fulana za rangi ya damu
ya mzee ambapo utaratibu wa kuvaa utakuwa ni suti kuvaliwa siku za wiki na
fulana kwa siku za mwisho wa juma.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi huo leo tarehe 6 Aprili, 2020 jijini Dar es Salaam, Waziri
Kamwelwe amesema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa huduma ya usafiri hasa kwa
kuzingatia kuwa zaidi ya asilimia 90 ya wafanyakazi na wafanyabiashara wa Mkoa
wa Dar es Salaam, wanategemea usafiri wa umma kufika kwenye maeneo yao ya kazi.
Mhe.
Kamwelwe amepongeza hatua ya uboreshaji wa sare hizo na kuwahimiza madereva na
makondakta kuzivaa sare hizo wakiwa kazini na kuzingatia usafi, unadhifu
na matumizi ya lugha nzuri zinazojali abiria wakati wa utoaji huduma za
usafiri.
Mkurugenzi
wa VETA Kanda ya Dar es Salaam, Leah Dotto amewashukuru viongozi wa DARCOBOA na
UWADAR kwa kuendelea kuiamini VETA kufanya kazi ya kushona sare za madereva na
makondakta wa dalalala ambapo kwa sasa wameweza kushona sare hizo mpya 6,000.
Amesema
kupitia ushonaji wa sare hizo katika Chuo cha VETA Dar es Salaam, VETA imeweza
kujenga nguvukazi iliyo tayari kuingia kwenye soko la ajira na kuanza kuzalisha
moja kwa moja kwa kuwa wahitimu wa fani ya ushonaji hutumika pia kufanya kazi
hiyo.
Dotto
amemuhakikishia Waziri Kamwelwe kuwa VETA ina uwezo mkubwa wa kushona sare
katika vyuo vyake vilivyosambaa nchi nzima na kuomba VETA iaminiwe kufanya kazi
hiyo hata katika maeneo mengine kulingana na mahitaji.
Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini – LATRA, Gilliad Ngewe amesema
mabadiliko ya sare hizo yamelenga kuboresha muonekano wa madereva na makondakta
wa jiji la Dar es Salaam.
Naye
Mwenyekiti wa UWADAR, Kismat Jaffar amewasihi madereva na makondakta kutumia sare
hizo mpya na kuwakikishia kuwa ubora wa sare hizo ni wa kiwango cha juu.
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (Mb), akizungumza wakati wa uzinduzi wa
sare mpya za madereva na makondakta wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam.
Muonekano
wa sare mpya za madereva na makondakta wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam. Sare
hizo zimeshonwa na Chuo cha VETA Dar es Salaam.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe (Mb), akionyesha
moja ya sare mpya za Madereva na Makondakta wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam,
wakati wa uzinduzi wa sare hizo leo tarehe 6 Aprili, 2020. Sare hizo zimeshonwa
na Chuo cha VETA Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment