CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Monday, 31 May 2021

CHUO CHA VETA CHATO KUWA CHA KWANZA KUTOA MAFUNZO YA UFUNDI STADI WA UVUVI NA UCHAKATAJI SAMAKI

 

Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Chato mkoani Geita kinatarajiwa kuwa chuo cha kwanza kuanza kutoa mafunzo ya Uvuvi na Uchakataji Samaki katika ngazi ya Ufundi Stadi nchini.Hayo yamebainishwa, tarehe 25 Mei 2021 wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa vya mafunzo ya stadi za Uvuvi na Uchakataji wa Samaki kwa ajili ya chuo hicho vilivyonunuliwa kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China. 

Katika hafla hiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako amesema kuwa ingawa vipo vyuo vinavyotoa mafunzo yanayohusiana na Uvuvi na Uchakataji Samaki katika ngazi za juu, hakukuwa na chuo kinachotoa mafunzo ya namna hiyo kwenye ngazi ya ufundi stadi.

Amesema kuanzishwa kwa mafunzo hayo kunatarajiwa kuwasaidia kwa kiasi kikubwa wananchi wa mikoa inayozunguka Ziwa Victoria kuboresha shughuli zao za kiuchumi ambazo zinahusiana na uvuvi na biashara ya samaki. 

“Miongoni mwa manufaa yanayotarajiwa ni kuongeza mavuno ya samaki na kuongeza thamani ya samaki na mazao yake,” amesema.

Ameagiza VETA kuendelea kupanua mafunzo hayo katika vyuo vingine, hasa vinavyozunguka maziwa, bahari na mito mikubwa ambako shughuli kubwa za wananchi wa mikoa hiyo ni uvuvi na biashara ya samaki.

Ameishukuru Serikali ya China kwa maendeleo nchini, hususani ile inayolenga kuboresha uendelezaji ujuzi na sekta ya elimu kwa ujumla.

Naye Naye Balozi wa China nchini, Wang Ke, amesema Serikali yake itaendelea kusaidia miradi mbalimbali ya elimu nchini kwani inatambua kuwa elimu ina mchango mkubwa sana katika kuongeza tija na kuchangia maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu amesema VETA itaendelea kupanua mafunzo hayo katika vyuo vingine hatua kwa hatua.

“Tunafungua ukurasa mpya Chato. Kama nasaha za Waziri zilivyotuasa, ni wakati wa kujipanga vyuo vilivyo katika maeneo ya wavuvi, hasa vinavyojengwa sasa, kama Mafia, Ukerewe, Kagera, Rufiji, Pangani, Nyasa, Uvinza, n.k. Na vikongwe pia kama Mwanza, Mara na Dar es Salam,” amesema.

Hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo ilifanyika kwenye ofisi za VETA Makao Makuu jijini Dar es Salaam na kuwahusisha Mheshimiwa Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mheshimiwa Wang Ke, Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania.

Viongozi na watendaji wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Dkt. Leonard Akwilapo, Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; Dkt. Ethel Kasembe, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Elimu ya Ufundi, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; Ndugu Peter Maduki, Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi; Wakurugenzi na Menejimenti ya Makao Makuu pamoja na Wakuu wa vyuo vya VETA vya Chato, Kipawa na Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu ndiye aliyekuwa mwenyeji wa tukio hilo.

Vifaa vilivyokabidhiwa vinatokana na ahadi iliyotolewa tarehe 7 Januari 2021 na Mheshimiwa Wang Yi, Waziri wa Mambo ya Nje ya China na Mjumbe wa Baraza la Taifa la nchi hiyo wakati wa Uzinduzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Chato. Kwa niaba ya Serikali yake, Mheshimiwa Yi aliahidi kutoa kiasi cha Yuan milioni moja karibu sawa na shilingi milioni 350 kwa ajili ya kununua vifaa vya Mafunzo ya Stadi za Uvuvi na Uchakataji Samaki kwa ajili ya Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Chato.



No comments:

Post a Comment