Jumla ya wakulima
2,176 (wanawake 1,294 na wanaume 882) wa mikoa ya Morogoro, Iringa na Njombe
wamenufaika na mafunzo ya stadi katika kilimo na ufugaji yaliyotolewa
kupitia mradi wa Tajirika na Kilimo unaotekelezwa na Mamlaka ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Shirika la Kimataifa la CARE na Taasisi ya
Ukuzaji Kilimo Uwanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT).
Akizungumza wakati wa
kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mradi jijini Dodoma, tarehe 22 hadi 23
Julai 2021, Mratibu wa Mradi huo kutoka VETA, Bw. Perecy Ugula, amesema
wakulima hao walipatiwa mafunzo ya ufugaji bora wa mifugo hasa ng’ombe wa
maziwa na kuku, kilimo cha mazao mchanganyiko, na kilimo cha mbogamboga na
matunda, na kufanikiwa kubadili uendeshaji wa shughuli zao hizo kuwa za kisasa
na za kibiashara.
Kwa mujibu wa Bw.
Ugula, mafanikio mengine yaliyopatikana kwenye mradi huo ni pamoja na uandaaji
wa mitaala miwili ya sekta ya Kilimo, ambayo ni Mtaala wa Kilimo cha Mbogamboga
na Matunda, Mtaala wa Kilimo cha Mazao, na kuuboresha mtaala wa Afya na Ufugaji
wa Mifugo.
Kwa upande wake,
Afisa Tathmini na Ufuatiliaji wa Shirika la Kimataifa la CARE, Bw. Edwin Sallu,
amesema kupitia utekelezaji wa mradi huo wamegundua uwepo wa uhitaji mkubwa wa
mafunzo ya stadi za kuboresha shughuli za kilimo kwa wakulima wadogowadogo
vijijini na kwamba wengi wao wako tayari kugharamia mafunzo hayo kama
inavyofanyika sasa katika Mradi wa Tajirika na Kilimo, hivyo akaiomba VETA
kupanua zaidi wigo wa mafunzo kwa mfumo wa kuwafuata wahusika katika maeneo yao
vijijini.
Sallu amesema mafunzo
hayo yamewezesha kuunda vikundi 141 vya uzalishaji katika sekta ya kilimo cha
mazao mchanganyiko, Mbogamboga na matunda na ufugaji wa kibiashara, ambapo kwa
sasa wanafanya shughuli zao za kilimo kwa umoja, hali inayowezesha uzalishaji
mazao kwa wingi, ubora na uhakika wa kufikia masoko ya bidhaa zao na kuwezesha
wakulima hao kukopesheka kwa urahisi na kupata faida nzuri.
“Kwa kweli
tumeshuhudia manufaa makubwa ya mafunzo yaliyotolewa kupitia mradi huu kwa
wakulima vijijini, hasa ukizingatia kuwa asilimia 67 ya wanufaika ni wanawake
na watoto wa kike ambao tunaamini wataleta mabadiliko chanya kwenye jamii zao,”
amesema.
Meneja wa Kongani ya
Kilombero kutoka Taasisi ya SAGCOT, Bw. John Nakei, amesema kuwa Taasisi yake
itaendelea kutoa ushauri, kuwaunganisha na fursa za masoko, na kutoa elimu
zaidi kwa wakulima katika mikoa hiyo ili kuwasaidia kuendesha shughuli hizo za
kilimo kwa tija zaidi na kuwezesha uzalishaji endelevu wa chakula.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt.
Kejeri Gillah, licha ya kuwapongeza wadau katika utekelezaji wa mradi huo,
ameshauri kuweka mkakati wa uendelezaji wa shughuli zilizofanywa kwenye mradi
huo ili wakulima wengi zaidi wanufaike na mafunzo hayo.
Mkurugenzi wa VETA
Kanda ya Nyanda za Juu, Bi. Susan Magani, amesema VETA inaendelea na jitihada
mbalimbali za kuhakikisha mafunzo ya ufundi stadi yanawafikia wananchi wengi
zaidi, hasa maeneo ya vijijini, na kwamba anaamini kuwa wakulima wengi zaidi
nchini watanufaika na mafunzo hayo ili kuboresha shughuli zao.
Mradi wa Tajirika na
Kilimo ulianza kutekelezwa mwaka 2018 kwa lengo la kujenga na kuimarisha ujuzi
katika sekta ya kilimo kwa wakulima 2,200 na unatarajiwa kumalizika
Desemba 2021.
No comments:
Post a Comment