Waziri wa Nchi Ofisi
ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye
Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama, amewataka viongozi wa mikoa na halmashauri
nchini kutoa kipaumbele cha mikopo kwa wahitimu wa ufundi stadi ili kuwawezesha
kujiajiri na kuajiri wengine.
Waziri Mhagama
ameyasema hayo Jumamosi, tarehe 31 Julai, 2021, alipotembelea na kukagua
shughuli za utekelezaji wa programu ya mafunzo ya Uanagenzi inayofadhiliwa na
Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu katika
Chuo cha VETA Busokelo, Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya.
“Nawaomba sana
viongozi wa mikoa na halmashauri mtoe kipaumbele cha mikopo kwa kwa hawa vijana
ili wapate mitaji na vifaa vya kufanyia kazi baada ya kuhitimu. Tena ukiwapa
hawa watachangia kuongeza mapato kwenye halmashauri yako na unakuwa na uhakika
wa mikopo yako kurejeshwa, maana tayari wana ujuzi,” amesema.
Awali, Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Dkt. Pancras
Bujulu, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwezesha vijana kupata mafunzo ya
ufundi stadi na ameahidi kuwa Mamlaka itahakikisha vijana hao wanapata mafunzo
bora yatakayowawezesha kujiajiri baada ya kuhitimu.
Akisoma taarifa ya
utekelezaji wa programu hiyo katika Chuo cha VETA Busokelo, Kaimu Mkuu wa Chuo
hicho, Bw. Wilbert Bendera, amesema jumla ya vijana 173 wa Halmashauri ya
Busokelo walipata fursa ya mafunzo hayo katika fani za Useremala, Ushonaji,
Umeme, Matumizi na Ukarabati wa Kompyuta na Utengenezaji Vifaa vya
Kielektroniki, ingawa hadi sasa walioripoti ni 127 tu, sawa na asilimia 74.
Kufuatia taarifa
hiyo, Waziri Mhagama ameagiza uongozi wa Chuo hicho kushirikiana kwa karibu na
Mbunge wa Jimbo la Busokelo, Uongozi wa Halmashauri ya Busokelo, pamoja na
Diwani wa Kata ya Lufilyo kuhakikisha nafasi za vijana ambao hawakuripoti
zinajazwa mara moja ili wana-Busokelo wanufaike na fursa hiyo.
No comments:
Post a Comment