Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP), liko mbioni kuanzisha chuo maalum cha ufundi stadi kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa akili katika eneo la Mlandizi, mkoani Pwani.
Naibu Katibu
Mkuu wa DMP anayeshughulikia Huduma za Jamii, Bi. Agnes Lema, alibainisha hayo Jumatano,
tarehe 1 Septemba 2021, katika kikao cha mashauriano na Menejimenti ya Mamlaka
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kilichofanyika kwenye ofisi za VETA
Makao Makuu, jijini Dodoma.
Amesema mpango
huo wenye lengo la kujenga fursa za ajira kwa watu wenye ulemavu wa akili
nchini Tanzania ulianza tangu mwaka 2012 na matayarisho kuanza rasmi mwaka
2017. Kwa sasa matayarisho hayo yamefikia hatua nzuri na hivyo wamedhamiria
kuhakikisha mafunzo yanaanza rasmi mwaka ujao, 2022.
“Kwa kweli
sisi tunaomba ushirikiano wenu katika nyanja zote. VETA mtupe miongozo,
ushauri, mitaala na kila kitu ambacho kitasaidia kuwezesha mpango huu wa
kusaidia vijana hawa kupata mafunzo unafanikiwa” amesema Bi. Lema.
Akitoa
wasilisho kuhusu Chuo hicho na mpango wa mafunzo, Mratibu wa Mradi wa Mradi
huo, Bi. Caroline Shedafa amesema kuwa wazo la kuanzisha chuo cha ufundi stadi
kwa watu wenye ulemavu wa akili lilianza mwaka 2012 kutokana na uzoefu wa
karibu miaka 40 ya utoaji elimu ya shule ya msingi kwa watu wenye ulemavu wa
akili na usonji, katika kituo cha Kanisa hilo kijulikanacho kama “Mtoni Deacon
Lutheran Centre”, kilichoko Mtoni jijini Dar es Salaam. Kituo hicho
kinaendeshwa na Kanisa hilo kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya
Temeke.
“Changamoto ni
kwamba, wanafunzi wengi wenye ulemavu wa akili na wanaosoma Kituo cha Mtoni,
baada ya kumaliza masomo yao, wanakosa mahali pa kwenda, kwani hakuna fursa ya
kuendelea na masomo ili kuendeleza ujuzi na stadi walizopata kituoni hapo au
katika vituo vingine ya aina hiyo. Hivyo, vijana hawa hushindwa kupata ajira au
kujiajiri. Kwa hiyo, vijana hawa hukaa tu nyumbani bila shughuli maalum na
kuendelea kuwa wategemezi,” amesema.
Bi. Shedafa
amesema Chuo cha Ufundi Stadi kwa Watu wenye Ulemavu wa Akili Mlandizi
kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa
kudahili wanafunzi 200 wa bweni na kitatoa kozi mbalimbali zikiwemo Utunzaji wa
Nyumba, Uandaaji Chakula, Upishi na Uokaji Mikate.
Ameongeza kuwa
wanafunzi watapewa fursa ya kwenda kufanya mazoezi ya kazi wakati wakiwa chuoni
ili kuanza kuwaandaa kwa kazi husika.
Mkurugenzi
Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu ameipongeza Dayosis ya Mashariki na Pwani ya
KKKT kwa mpango huo, kwani vijana wengi wenye ulemavu wa akili wamekuwa na
fursa finyu katika mafunzo ya ufundi stadi, ingawa wakipata mafunzo hayo
wanaonekana kuyamudu na kufanya vyema.
No comments:
Post a Comment