Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim
Majaliwa ameeleza kuguswa na mchango wa Prof. Mark Mwandosya katika kuwezesha
utoaji mafunzo ya ufundi stadi mkoani Mbeya kwa kuipa serikali majengo
aliyokuwa akiyamiliki ili yabadilishwe na kuwa chuo cha ufundi stadi.
Mwaka 2017, Prof. Mwandosya na familia yake walitoa majengo
yaliyokuwa ya kituo chao cha kulelea watoto yatima cha ‘Lucy Hope Centre’ na
kuyakabidhi kwa VETA ili kuanzisha chuo cha ufundi stadi.
Akizindua Chuo cha VETA Busokelo tarehe 1 Agosti 2021, Mhe.
Majaliwa alimshukuru Profesa Mwandosya na familia yake kwa kitendo hicho cha
kizalendo na kueleza kuwa Chuo hicho kitasaidia sana vijana wa Halmashauri ya Wilaya
ya Busokelo na maeneo mengine mkoani Mbeya kujipatia ujuzi na kuanzisha
shughuli zao mbalimbali za kiuchumi.
“Jambo mlilolifanya si jambo dogo na wala siyo jambo rahisi kwa
watu wengine ila ni kwa watu wenye maono ya mbali na mapenzi mema… Mlichokifanya
hakitasahaulika na hatuna namna ya kuwashukuru wala fedha ya kuwalipa kufidia kwa
jambo hili, bali shukrani zetu ni kuendelea kuiheshimu familia ya Prof
Mwandosya,”alisema Majaliwa
Mhe. Majaliwa alitumia fursa hiyo kuwasihi vijana wa Busokelo
waliopata fursa ya ufadhili wa Serikali kupitia programu maalumu ya mafunzo ya
ufundi stadi kwa ufadhili wa Ofisi yake watumie vizuri fursa hiyo ili
wanufaike.
Alisema zaidi ya vijana 45,000 wanaendelea na mafunzo katika vyuo
vya ufundi stadi nchini ili wajipatie ujuzi kwenye maeneo mbalimbali kwa miezi
sita ambapo Serikali imelipia ada ya mafunzo kwa asilimia 100.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu alisema chuo
hicho kina uwezo wa kudahili wanafunzi 120 kila mwaka kwa kozi za muda mrefu na
320 kwa kozi za muda mfupi kwa mwaka.
Alisema kupitia programu ya ufadhili wa Ofisi ya Waziri Mkuu, chuo
cha VETA Busokelo kimedahili wanafunzi 127 katika fani za Useremala, Ushonaji,
Umeme wa Majumbani, ukarabati wa Vitarakimishi (Computer Maintanance) na
Utengenezaji wa vifaa vya kielektroniki.
No comments:
Post a Comment