Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi Stadi (VETA) imeingia makubaliano ya kushirikiana na Shirika la REDESO
kuwapatia elimu na stadi za matumizi ya nishati safi, vijana na wanawake zaidi
ya 3,000.
Hati ya makubaliano ya ushirikiano huo imesainiwa jana, tarehe 26 Machi , 2025, katika ofisi za VETA Makao Makuu jijini Dodoma ambapo mafunzo hayo yatatolewa katika vyuo vya VETA nchini.
Akizungumza baada ya zoezi la
utiaji saini, Mtendaji Mkuu wa Redeso, Abeid Kasaizi, amesema pamoja na mradi
huo kuwapatia ujuzi vijana na wanawake katika maeneo mbalimbali nchini kupitia
mafunzo rasmi ya VETA na pia makubaliano hayo yanajumuisha mafunzo kwa walimu
wa VETA kuhusu nishati safi, utayarishaji wa mitaala maalum, pamoja na
upatikanaji wa vifaa vya kufundishia.
"Mafunzo haya yatawasaidia kupunguza matumizi ya nishati chafu, hivyo kusaidia uhifadhi wa mazingira na kupunguza utoaji wa hewa ya ukaa," amesema Kasaizi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu
wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema kuwa Serikali chini ya uongozi wa Mhe.
Rais Samia Suluhu Hassan imeweka mkazo na kipaumbele katika matumizi ya nishati
safi na kwamba VETA inaendelea kuweka na kutekeleza mipango ya matumizi ya
nishati safi.
"Sisi VETA tumeona umuhimu wa kuendeleza elimu ya matumizi ya nishati safi ili kuhakikisha wananchi wanapata ujuzi wa kuzalisha na kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira, tunatarajia kupitia mafunzo haya, wananchi wataweza kutengeneza na kutumia nishati safi na hivyo kujipatia fursa za ajira na kuchangia maendeleo endelevu ya taifa,"amesema.
No comments:
Post a Comment