CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Friday 4 May 2018

VETA DAKAWA YAANZA KUTOA MAFUNZO YA UFUGAJI BORA WA NYUKI

Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi cha VETA Dakawa kimeanza kutoa mafunzo ya ufugaji bora wa kisasa wa nyuki.

Mkuu wa chuo cha VETA Dakawa Beatus Nyakunga amesema kuwa mafunzo hayo yameanza kutolewa kwa muda mfupi ambapo kijana anaweza kujiunga na kupata utaalam wa kutengeneza mizinga na kufuga nyuki kisasa kwa muda wa wiki mbili.

Kwa mujibu wa Bw. Nyakunga, mafunzo wanayoyatoa ni ya ufugaji bora na wa kisasa wa nyuki na kwamba mizinga ya nyuki huwekwa kwenye mabanda badala ya kutundika kwenye miti.

Amesema chuo chake kimeamua kuanzisha mafunzo hayo kutokana na ukweli kuwa mazao yanayotokana na nyuki yanaendelea kupanda thamani kila siku na kwamba ni fursa nzuri sana kwa vijana kujiajiri.

“Tunaamini kuwa mafunzo haya yatasaidia vijana wengi kujiajiri wenyewe kwa sababu mazao ya nyuki yana faida sana…Mzinga mmoja unaweza kutoa kiasi cha chini cha kilo 10 na kilo moja ni shilingi 10,000 hadi 15,000”Alisema.
Anasema tayari wameshavuna kilo 72 kutoka kwenye mizinga nane mwaka huu na kwamba mizinga mingine 53 ina nyuki wanaoendelea kuchakata na kwamba wanatarajia kuvuna mwishoni mwa mwezi huu (Aprili, 2018) na mavuno mengine ni mwezi Julai.

Bw. Nyakunga anawahamasisha vijana na jamii kwa ujumla kuhamasika na mafunzo hayo na kuweza kujiunga nayo kama njia mojawapo ya kujiongezea kipato huku akibainisha kuwa ni vijana 15 tu ambao wameshasomea mafunzo hayo kwa mwaka huu.

Naye mtaalamu wa ufugaji nyuki chuoni hapo Bw. Yohana Mkonongo anasema ufugaji wa nyuki kwa kukusanya mizinga kwenye banda una faida zaidi na uhakika wa mavuno tofauti na ule wa kutundika mizinga kwenye miti ambapo mizinga mingi huharibiwa na wanyama pamoja na wadudu, hunyeshewa na mvua na wakati mwingine kuungua moto.


No comments:

Post a Comment