Naibu Waziri wa
Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ameiagiza Mamlaka ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kuboresha usimamizi na uthibiti wa vyuo
vinavyotoa elimu ya Ufundi Stadi nchini ili kuzalisha mafundi wenye ubora.
Akizungumza wakati wa
ziara yake katika ofisi za VETA Makao Makuu jijini Dar es Salaam Jumanne tarehe
16 Oktoba 2018, Ole Nasha alisema elimu ya ufundi stadi
inategemewa sana katika kutekeleza azma ya serikali ya kufikia uchumi wa kati
kupitia viwanda hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuboresha usimamizi wa vyuo
vinavyotoa elimu hiyo.
Aliagiza uhakiki
ufanyike katika vyuo vyote nchini ili kubaini vyuo ambavyo vinatoa mafunzo bila
kufuata kanuni na sheria za utoaji mafunzo na hatua za kisheria ikiwemo kufungia
vyuo hivyo zichukuliwe.
“Naagiza vyuo vyote
vinavyotoa elimu ya ufundi stadi kuhakikisha vina usajili na ithibati… Hatuwezi
kuwa na elimu bora kama hatuna vyuo vyenye ubora vitakavyozalisha nguvu kazi
bobezi ya uchumi wa viwanda” Alisema
Ole Nasha aliitaka
VETA pia kupitia mara kwa mara mitaala ya kufundishia ili kuhakikisha mafunzo
yanayotolewa yanaendana na mahitaji ya soko kwa wakati husika.
Katika hatua
nyingine, Ole Nasha aliipongeza VETA kwa jitihada ilizoanza kuzichukua katika
kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali hasa ya ujenzi wa vyuo vya Mikoa na
Wilaya na kuitaka kutosita kusitisha mkataba na Mkandarasi atakayeenda kinyume
na makubaliano ya mkataba.
Awali, Mwenyekiti wa
Bodi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Peter Maduki alisema VETA inaendelea
na jitihada za kupaua wigo wa utoaji mafunzo kupitia ujenzi wa vyuo vya Mikoa
na Wilaya lengo likiwa kuhakikisha idadi ya udahili inaongezeka kutoka 200,000
hadi 700,000 ifikapo mwaka 2020.
Naye Mkurugenzi Mkuu
wa VETA Dkt. Pancras Bujulu alisema kuwa Mamlaka hiyo itaendelea kubuni mbinu
mbalimbali za kuhakikisha elimu ya ufundi stadi inafikia watanzania wengi zaidi
kwa ubora unaokubalika.
Alisema Mamlaka hiyo
inatambua wajibu mkubwa iliyonayo katika kuandaa nguvu kazi yenye stadi mahiri
ili kushiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa viwanda.
Katika ziara hiyo,
Naibu Waziri alikutana na wafanyakazi wa VETA na kuwasisitiza uwajibikaji na
uadilifu katika kutekeleza majukumu yao
No comments:
Post a Comment