Wasomi
wa vyuo vikuu nchini wameshauriwa kujifunza ufundi stadi ili kujiongezea ujuzi
na ubunifu utakaowawezesha kujiajiri.
Ushauri
huo umetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Walimu wa Ufundi Stadi
Morogoro (MVTTC), Profesa Elifas Bisanda wakati wa uzinduzi wa
Baraza hilo tarehe 15 Novemba 2018.
Profesa
Bisanda, ambaye pia ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria amesema ni vyema wasomi
nchini wakaondokana na dhana ya kuwa usomi ni kuajiriwa katika maofisi na
badala yake watumie usomi wao katika kujiongezea ujuzi wa ufundi stadi ambao
wanaweza kuutumia kubuni miradi na huduma ambazo zitasaidia kutatua changamoto
mbalimbali katika jamii huku zikiwanufaisha wao kwa kipato.
Amesema
kwa kuzingatia mkakati na mwelekeo wa nchi kwenye uchumi wa viwanda miongoni
mwa mikakati ya VETA itakuwa ni kuwahamasisha vijana hao wasomi wanaomaliza
vyuo vikuu ambao wanatafuta ajira kuingia kwenye mafunzo ya ufundi stadi ili
wawe na uwezo wa kubuni vitu mbalimbali hata kama wamesomea kozi nyingine.
Amesema
wahitimu wa vyuo vikuu wakiongezea maarifa yao na ujuzi kutoka vyuo vya ufundi
stadi itakuwa rahisi kujiajiri na
kufikia malengo yao.
Profesa
Bisanda alitoa mfano wa nchi ya Korea ambapo wahitimu wengi wa vyuo vikuu katika
nchi hiyo ndio wanaojiunga na vyuo vya ufundi na kwamba asilimia 95 ya
wanafunzi wanaojiandikisha darasa la kwanza kwa nchi hiyo wanamaliza elimu cha
chuo kikuu tofauti na hapa nchini ambapo ni asilimia 4 pekee ndio wanaofika
ngazi ya chuo kikuu.
“Nchi
ya Korea huwezi kuwa mwalimu bila kuwa na degree na ndio wanaoenda vyuo vya
ufundi, lakini huku kwetu wanaofeli darasa la saba ndio wanaojiunga na vyuo vya
ufundi stadi. Ifikie mahali mifumo yetu ya Tanzania ibadilike ili kuhakikisha
tunapata ufanisi na ujuzi kwa watoto wetu,”alisema Profesa Bisanda
Akizungumza
na wajumbe wa Baraza hilo la Chuo cha ualimu na ufundi stadi (MVTTC)Morogoro
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Lukas Mwaisaka kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa
wa Morogoro Dk Steven Kebwe, amewakumbusha jukumu lao katika kusimamia vyema
chuo hicho maalum kwa ajili ya walimu wa ufundi stadi, ili kiweze kutoa walimu
bora watakaohamisha ujuzi wao kwa wanafunzi wa ufundi stadi katika vyuo
mbalimbali nchini.
Amesema
jukumu la MVTTC ni kubwa kwa kuwa ni chuo pekee cha mafunzo ya Walimu wa Ufundi
Stadi nchini huku vyuo vya ufundi stadi vikiwa ni 550 sasa na bado kuna vingine
vinatarajiwa kuanzishwa muda si mrefu.
Amesema
kuwa matumaini ya Serikali ni kuona chuo hicho pamoja na kutoa mafunzo kwa
waalimu wa ufundi stadi pia kinatoa
mafunzo kwa viongozi wa vyuo vya ufundi stadi ili wawe na sifa pekee za
kusimamia utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu aliwaagiza watendaji
wa MVTTC kufikiria kuandaa walimu wenye stadi za kufundisha watu wenye ulemavu
kwa kuwa sasa VETA inakabiliwa na changamoto za ufundishaji ufundi stadi kwa
watu wenye ulemavu.
Aliwaomba
wajumbe wa Baraza la MVTTC kukishauri chuo hicho na kuhimiza kuanzisha mipango
na mikakati mbalimbali ya kuanza kuandaa walimu wa ufundi stadi katika mwelekeo
wa kufundisha watu wenye uemavu.
No comments:
Post a Comment