Wadau
wa Mradi wa Mafunzo Jumuishi ya Ujuzi kwa Ajili ya Sekta ya Madini (Integrated
Mining Technical Training-IMTT) wamekubaliana kuukuza na kuupanua mradi huo ili
uwe Mpango maalum wa mafunzo utakaohusisha sekta na wadau mbalimbali zaidi ya
makampuni ya madini. Mradi huo unaoendeshwa kwa mfumo wa uanagenzi kupitia chuo
cha VETA Moshi uliasisiwa na makampuni ya uchimbaji madini kupitia Chemba ya
Nishati na Madini Tanzania(TCME) kwa ushirikiano na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo
ya Ufundi Stadi (VETA).
Wazo
la kubadili mradi huo kuwa mpango maalum lilijadiliwa na kuafikiwa tarehe 2
Novemba, 2018 katika kikao cha pamoja cha Kamati ya Uwakilishi katika Usimamizi
wa Mradi (Representative Management Committee-RMC) inayoundwa na wadau wa mradi huo ambao ni pamoja na Mamlaka
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA); Chemba ya Nishati na Madini
Tanzania(TCME); Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; na Wawakilishi wa
Makampuni ya Madini.
Katika
kikao hicho kilichafanyika kwenye chuo cha VETA Moshi chini ya Uwenyekiti wa
Janet Reuben kutoka TCME, wadau walijadili na kuzingatia ukweli kuwa tangu
kuanzishwa kwake mwaka 2008, mradi huo umezidi kukua na kupanuka katika katika
utoaji wa mafunzo huku makampuni zaidi hata yale ya yasiyohusika na madini
yakizidi kujiunga, hivyo tafsiri kuwa mradi huo ni maalum kwa mafunzo kwa ajili
ya kusaidia sekta ya madini pekee kuzidi kufifia.
Wadau
hao walikubaliana kuwa hata jina libadilike na kuwa Mpango wa Mafunzo Jumuishi ya
Ufundi (Integrated Technical Training Programme-ITTP).
“kwa
kweli mradi umepanuka sana na wadau wengi wamejiunga na wengine wanaendelea
kuonesha nia ya kujiunga kutoka sekta mbalimbali. Kwa hiyo hata uhalali wa
kuendelea na jina la awali la IMTT unaanza kukosekana,” alisema Shayo Simon,
Makamu wa Rais anayehusika na Uendelevu kutoka kampuni ya Geita Gold Mining
Tanzania-GGM.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt.
Pancras Bujulu licha ya kuwashukuru wadau kuendelea kusaidia vijana kupata mafunzo
kupitia mradi huo, alisema kuwa VETA iko tayari kuendelea na mafunzo hayo
katika utaratibu wa kuwa na Mpango mmoja ambamo makampuni na wadau kutoka sekta
mbalimbali watakuwa wakiingia na miradi ya vipindi tofauti tofauti.
Akiwasilisha
taarifa ya maendeleo ya IMTT, Mratibu wa Mradi huo Theresia Mosha alisema kuwa
katika kipindi cha kuanzia mwaka 2009 hadi 2018 mradi ulidahili jumla ya
wanagenzi 825 katika fani mbalimbali ambapo 448 walihitimu, 265 wakiwa bado
wako mafunzoni na 112 waliacha mafunzo.
Mradi wa IMTT
ulianzishwa mwaka 2008 kwa ushirikiano kati ya VETA na TCME kwa madhumuni ya
kutoa mafunzo bora kwa ajili ya kusaidia sekta ya madini; kuzalisha mafundi
stadi mahiri watakaochangia maendeleo na ukuaji wa uchumi wa Tanzania; kukuza
mahusiano baina ya vyuo na waajiri kama
migodi na sekta nyingine pamoja na Kutoa mafundi wenye utaalamu unaoendana na teknolojia ya kisasa. Mafunzo
hayo huendeshwa kwa mfumo wa uanagenzi ambao unahusisha mafunzo kwa kupokezana
kati ya chuo na mahala pa kazi katika mzunguko kipindi chao chote cha mafunzo.
No comments:
Post a Comment