Chuo
cha Ufundi Stadi Kagera (VETA Kagera) kina mpango wa kuanzisha mafunzo ya
Ufugaji, Uandaaji na Uhifadhi wa samaki ili
kwenda sambamba na mazingira na shughuli za kiuchumi zinazoendeshwa na wakazi
wanaokizunguka chuo hicho pamoja na mkoa wa Kagera na mikoa ya kanda ya Ziwa kwa
ujumla.
Mkuu
wa Chuo cha VETA Kagera, Baluhi Mitinje aliyabainisha hayo hivi karibuni wakati
wa ziara ya Menejimenti ya VETA katika chuo hicho.
Alisema
sehemu kubwa ya Mkoa wa Kagera iko kandokando au imezungukwa na Ziwa Victoria
na shughuli nyingi za uvuvi zinafanyika katika mkoa huo, hivyo chuo chake
kimeona ipo fursa na haja ya kujengea ujuzi wakazi wa Kagera na mikoa ya jirani
katika ufugaji na usindikaji wa samaki.
Alisema,
ujuzi utakaofundishwa ni wa ufugaji kwa kutumia vizimba-cages na kuandaa na
kuhifadhi samaki kwa njia ya kubanika kwa kutumia matanuru ya kisasa.
“Ukiangalia
eneo kubwa la Kagera limezungukwa na ziwa na shughuli za wananchi zinahusiana
na uvuvi, kwa hiyo tumeona tuitumie fursa hii kwa kuwapa ujuzi ili waweze
kuboresha shughuli zao,” alisema.
Alisema
mafunzo hayo yanatarajiwa kuanzishwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Uendelezaji Ujuzi
(Skills Development Fund-SDF) unaoratibiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA)
ambapo VETA Kagera iliandaa andiko na kufanikiwa kupata fedha za mradi wa
kuanzisha mafunzo hayo.
Sambamba
na mafunzo yanayohusiana na samaki, Mitinje aliongeza kuwa chuo hicho pia
kinapanga kuanzisha mafunzo ya muda mfupi katika ujuzi wa Ususi na Urembo
(Cosmetology); Umeme wa Jua (Solar); Utengenezaji wa Mashine za Ofisi; Ukarimu
kwa Wageni (Hospitality); Ufundi Bomba
(Plumbing); na kuimarisha zaidi mafunzo ya udereva wa magari.
Chuo
cha Ufundi Stadi Kagera (VETA Kagera) kilianzishwa mwaka 1987 chini ya Idara ya
Mafunzo na Majaribio ya Idara ya Ufundi iliyokuwa ndani Wizara ya Kazi na
Ustawi wa Jamii. Chuo kilianza kwa uwezo wa kudahili wanafunzi 120 kwa mwaka
kwa fani nne ambazo ni Useremala, Uashi, Ushonaji wa Nguo na Uungaji Vyuma.
Sasa
chuo hicho kimefikia uwezo wa kudahili wanafunzi zaidi ya 300 katika fani za
muda mrefu na zaidi ya wanafunzi 800 kwa kozi za muda mfupi kwa mwaka katika
fani sita za Ufundi wa Magari, Umeme,
Useremala, Uashi, Ushonaji wa Nguo na Uungaji Vyuma.
No comments:
Post a Comment