Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Dkt Pancras Bujulu amewahimiza
walimu wa ufundi stadi kuweka mkazo katika ujuzi na ubunifu kwenye utoaji wa
mafunzo ili kuwezesha kutoa wahitimu mahiri na wabunifu, hivyo kuonesha thamani
ya mafunzo yatolewayo chuoni na kuvutia vijana wengi zaidi kujiunga na elimu na
mafunzo ya ufundi stadi.
Akizungumza
na walimu na wafanyakazi wa chuo cha VETA Kagera, Oktoba 29, 2018 baada ya
kufanya ziara katika chuo hicho, Dkt Bujulu aliwaasa walimu kuwiwa zaidi kutoa
ujuzi na maarifa waliyonayo kwa wanafunzi na kusema kuwa ujuzi katika fani ni suala
la msingi zaidi kuliko hata juhudi za kumuwezesha mwanafunzi kufaulu mtihani, kwani
ujuzi ndio utakaowawezesha wanafunzi kutenda kazi baada ya kuhitimu.
“Kufaulu mtihani ni ishara ya ujuzi, lakini
haitoshi maana inategemea siku ile uliamkaje, mtihani ulitungwaje, ilitungwa
mada ipi ambayo ulijiandaa kuliko nyingine, lakini ujuzi ulioupata ni wa msingi
zaidi kwa kuwa unakwenda kuufanyia kazi kuliko mtihani uliofaulu,” alisema.
Alisema
mwanafunzi aliyepo chuoni akipewa ujuzi bora, maarifa na mwanga zaidi wa kuweza
kupambanua mambo kutamwezesha kuwa mbunifu pia na kumtofautisha na yule
aliyejifunza kupitia mfumo usio rasmi.
Alifafanua
kuwa hata fani ambazo udahili wake ulionekana uko katika kiwango cha chini
unaweza kuongezeka iwapo watu watabaini kuwa mafunzo chuoni ni bora zaidi
kuliko yale ya mtaani.
Aliongeza
kuwa kuna watu wenye mtazamo kwamba baadhi ya fani hazihitaji kwenda chuoni
kujifunza, kwani unaweza kujifunza mtaani na kuwa na ujuzi sawa tu na
aliyekwenda chuoni na kusema kuwa mtazamo huo unaweza kuondolewa kwa mhitimu wa
chuo cha ufundi stadi kuonesha umahiri, ubunifu na uwezo wa kupambanua mambo
kwa undani zaidi kuliko aliyejifunz mtaani.
Akielezea
maendeleo ya chuo cha VETA Kagera, Mkuu wa Chuo hicho Baluhi Mitinje alisema licha
ya chuo hicho kufanikiwa kuongeza udahili hadi kufikia wanafunzi 302 katika
daraja la 1, la 2 na la 3, baadhi ya fani ikiwemo ushonaji na useremala
zimekuwa na mwitikio mdogo wa vijana kujiunga nazo.
Alisema
fani hizo zinakosa sifa ya kupendwa na vijana na akatoa mfano wa takwimu
za mwaka 2018 ambapo fani ya Ushonaji
imedahili jumla ya wanafunzi 21 tu katika ngazi zote za 1, 2 na 3 huku
Useremala nako wakidahiliwa jumla ya wanafunzi 23 tu katika ngazi zote tatu.
Chuo
cha Ufundi Stadi Kagera ni miongoni mwa vyuo vitatu vinavyomilikiwa na VETA
vilivyopo Kanda ya Ziwa, ambacho kwa sasa kinatoa mafunzo katika fani za Ufundi
Magari, Umeme, Useremala, Uashi, Ushonaji nguo na Uungaji vyuma.
No comments:
Post a Comment