Waziri
Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amevutiwa na mafunzo yanayotolewa na Mamlaka
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kusaidia sekta ya madini.
Waziri
Mkuu alibainisha kuvutiwa kwake na kushangazwa na umahiri wa wanafunzi wa VETA
baada ya kutembelea banda la VETA tarehe 30 Septemba, 2018 katika maonesho ya
Teknolojia ya Uchimbaji na Uwekezaji kwenye Madini ya Dhahabu yaliyokuwa
yakifanyika katika viwanja vya Kalangalala, mjini Geita kuanzia tarehe 24 hadi
30 Septemba, 2018.
Akitembelea
mabanda kabla ya kufunga rasmi maonesho hayo, Waziri Mkuu alipita banda la VETA
na kupata maelezo kutoka kwa Meneja Uhusiano wa VETA, Sitta Peter juu ya
mafunzo mbalimbali yanayotolewa na VETA yanayogusa sekta ya madini ikiwa ni pamoja na ufundi wa mitambo
mikubwa, uendeshaji mitambo mikubwa, ulipuaji wa miamba na ukataji na
ung’arishaji madini ya vito, kisha kujionea umahiri wa wanafunzi wa VETA katika
stadi mbalimbali.
Miongoni
mwa yaliyomvutia zaidi ni ustadi aliouonesha mwanafunzi wa VETA Shinyanga
katika fani ya Ukataji na Ung’arishaji Madini ya Vito, Jesca Jonathani Nkani
alipokuwa akionesha namna ukataji na ung’arisha madini unavyofanyika, pamoja na
ujuzi wa uendeshaji mitambo mikubwa uliooneshwa na mwanafunzi wa VETA Moshi
katika programu Mafunzo ya Ufundi kwa Ajili ya Uchimbaji Madini (IMTT), Careeen
Vedasto.
Pamoja
na kueleza kufurahishwa kwake wakati akiwa katika banda la VETA, Waziri Mkuu
alibainisha pia katika hotuba yake ya ufungaji ambapo licha ya kuipongeza VETA
kwa kuanzisha mafunzo hayo, aliwahamasisha wananchi, hususani vijana kujifunza
ujuzi huo ambao unapatikana nchini.
Alisema,
kwa muda mrefu imekuwa ikidhaniwa kuwa teknolojia ya ukataji na ung’arishaji
madini inapatikana nje ya nchi tu na wale wanaoiendesha hapa nchini ni wageni
tu, kumbe ujuzi huo sasa unatolewa katika vyuo vya hapa nchini na kwamba
Watanzania wanaweza kujifunza na kuendesha shughuli za kuongezea thamani madini
hapahapa nchini.
“Nilivutiwa
sana na yule binti alivyokuwa aking’arisha madini kwa ustadi, nilitamani
ninunue moja, lakini alinieleza hizo ni kwa ajili ya mafunzo…………” alisema.
Aliwaasa
wananchi kutumia mafunzo mbalimbali yanayotolewa na VETA ili kuongeza tija
katika uchimbaji na uchakataji wa madini.
Kwa
upande wake, Waziri wa Madini, Angela Kairuki alieleza kuwa Wizara yake
itawasiliana na VETA na Kituo cha Utambuzi na Ukataji Madini ya Vito (TGC)
kuona namna ya kuweza kuwa na ushirikiano na kusaidiana katika eneo la
utambuzi, ukataji na ung’arishaji madini ya vito.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko aliiomba VETA kupunguza
wasiwasi wa wahitimu wa kozi ya Ukataji na Ung’arishaji madini juu ya suala la kupata
ajira kwa kuwa sheria na taratibu zilizowekwa na serikali sasa zinawabana wawekezaji,
kiasi kwamba watalazimika kuajiri wahitimu wengi wa hapa nchini.
“ili
upate dealer license (leseni ya uwakala), unapaswa uwe na mashine zisizopungua
30 na wataalam wa kuzitumia hizo mashine, na utaalam tunaoutaka ni ule wa mtu
aliyefuzu na cheti ndo uthibitisho. Sasa hawa wataalam watawapata wapi kama si
kutoka kwenu VETA?,” alisema na kuhoji.
No comments:
Post a Comment