Mashindano
ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu yamezinduliwa rasmi tarehe 14
Novemba 2018 huku Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ikipewa
jukumu la kuratibu mchakato wa mashindano katika makundi mawili ambayo ni Wabunifu
wa Ufundi Stadi na Wabunifu wa kutoka Sekta Isiyo Rasmi, hivyo kupata majina
matano ya kila kundi kuingia kwenye fainali.
Akizindua
mashindano hayo sambamba na Mwongozo wa Kuendeleza Ugunduzi, Ubunifu na Maarifa
Asilia, kwenye Ukumbi wa Kambarage, Nyerere square jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,
Profesa Joyce Ndalichako alisema mashindano hayo yataongozwa na kaulimbiu ya “Kukuza Ujuzi na
Ubunifu kwa Uchumi wa Viwanda.” na yatahusisha makundi mbalimbali ya
wabunifu wa kisayansi, teknolojia katika maeneo na nyanja mbalimbali nchini
kote, ambapo kilele chake kitakuwa Januari 2019.
Alisema ili nchi yetu iweze kunufaika na matokeo ya ubunifu,
uvumbuzi na maarifa asilia, kuna umuhimu wa kuwahamasisha wagunduzi, wabunifu
na wamiliki wa maarifa asilia.
“Kwa hiyo, mashindano
haya yatasaidia kuibua vipaji na kuhamasisha uendelezaji wa teknolojia na
ubunifu utakaoweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo endelevu ya
viwanda, kuongeza tija ya uzalishaji wa malighafi, kuongeza thamani ya bidhaa
zinazozalishwa nchini pamoja na kuboresha shughuli nyingine za kiuchumi. Kutokana na kutambua umuhimu wa sayansi, teknolojia na
ubunifu, Wizara yangu ina mpango wa kufanya mashindano haya yafanyike kila
mwaka ili uibuaji wa vipaji vya namna hii uwe endelevu, ” alisema.
Aliongeza kuwa Mwongozo wa Kuendeleza Ugunduzi, Ubunifu na
Maarifa Asilia utakuwa ni nyenzo ya kuongeza ufanisi wa taasisi
zinazoshughulikia masuala ya ugunduzi, ubunifu na umiliki wa maarifa asilia.
Akifafanua
juu ya umuhimu wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kwa maendeleo na ustawi wa
taifa Profesa Ndalichako alisema Sayansi, Teknolojia na Ubunifu zimeleta mapinduzi
makubwa katika sekta mbalimbali kama vile habari, biashara, viwanda na huduma
mbalimbali za kijamii huku akitoa mfano wa mabadiliko katika huduma za kifedha
yaliyosababishwa na ubunifu wa matumizi ya teknolojia ya simu za kiganjani.
Alisema
mchakato wa mashindano hayo utaratibiwa kwa ushirikiano
wa Kurugenzi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ya Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia; Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH); Taasisi ya
Teknolojia (DIT); Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na Ofisi
ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Mashindano hayo yatahusisha jumla ya makundi sita ambayo ni
Wabunifu kutoka Shule za sekondari wakiratibiwa na TAMISEMI; Wabunifu wa Ufundi
Stadi na Wabunifu wa Sekta Isiyo Rasmi wakiratibiwa na VETA; Wabunifu wa Ufundi
wa Kati wakiratibiwa na DIT; na Wabunifu wa Vyuo Vikuu na Wabunifu wa Taasisi
za Utafiti wakiratibiwa na COSTECH.
Awali
kabla ya kumkaribisha Waziri, Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia, Daktari Leonard Akwilapo, alitaja malengo mahususi ya mashindano
hayo kuwa ni pamoja na Kuibua na kutambua ubunifu mahiri nchini katika eneo la
sayansi na teknolojia; Kukuza hamasa ya ubunifu katika nyanja ya sayansi na
teknolojia; Kuhamasisha matumizi ya sayansi, teknolojia, ubunifu na hisabati
katika shughuli za kiuchumi na kijamii; Kuchochea
ugunduzi na ubunifu wa kisayansi na teknolojia utakaotegemeza maendeleo ya
uchumi wa viwanda; na Kushirikisha wadau ili kupata mawazo ya jinsi
sayansi, teknolojia na ubunifu yanavyoweza kuchangia katika kujenga uchumi wa
viwanda.
Alisema wabunifu bora watano kutoka katika kila kundi
watachaguliwa katika mchujo wa awali ili kuingia katika mashindano ya fainali
yatakayofanyika jijini Dodoma ili kupata washindi watatu wa fainali.
Naomba kusoma ufundi wa kutengeneza mageti ila elimu yangu ni darasa la saba naruhusiwa kusoma?0743788246
ReplyDelete