Mhitimu wa Chuo cha
VETA Dar es Salaam, Fidelis Christian Mchana ameibuka mshindi wa kwanza katika
kundi la Wabunifu wa Vyuo Vya Ufundi Stadi katika fainali za Mashindano ya
Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) yaliyohitimishwa leo
tarehe 7 Machi 2019 katika Viwanja vya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (Nyerere
Square) jijini Dodoma.
Fidelis alishiriki
mashindano hayo akiwa na ubunifu wa benchi linaloweza kugeuzwa kuwa meza ya
majadiliano na wakati mwingine kuwa meza ya kuchorea (Drawing Table) ambalo
katika maonesho hayo watu wamelibatiza jina la Benchi la Maajabu.
Kijana Fidelis amefuatiwa
na Mwalimu Emmanuel Bukuku kutoka VETA Dar es Salaam aliyeshika nafasi ya pili
na Mwalimu Sussack Mbulu wa VETA Songea aliyeshika nafasi ya tatu.
Mwalimu Emmanuel
Bukuku amebuni mfumo wa kutoa ishara ya sauti kwa watumiaji wa barabara wakati
Gari Moshi (train) linapokaribia kwenye makutano ya barabara na reli, lengo
likiwa ni kusaidia kupunguza ajali zinazotokana na magari au watu kugongwa na
Gari Moshi katika makutano ya barabara na reli.
Kwa upande wake,
Mwalimu Sussack Mbulu amebuni kifaa cha umwagiliaji (sprinkler) kilicho imara
na kinachoweza kuhudumia eneo kubwa na kwa ufanisi mkubwa.
Washiriki wengine
kutoka Kundi la Vyuo vya Ufundi Stadi waliofika fainali za mashindano hayo ni
Kintu Kilanga (VETA Dar es Salaam) aliyebuni kifaa ya usaili wa watoto wenye
ulemavu wa akili; Elly Maduhu (VETA Mara) aliyebuni mashine rahisi ya kuungia
vyuma; Aneth Mganga (VETA Kipawa) aliyebuni mfumo wa usalama kwa watumiaji wa
pikipiki; Edward Lunyilija (VETA Kigoma) aliyebuni kifaa cha kufukuza mbu; Patrick Jovenary (kutoka Mfumo wa Mafunzo ya
Uanagenzi VETA Dar es Salaam) aliyebuni mfumo wa usalama majumbani, kwenye
magari na lifti za majumba marefu na Lawrance Mashindano (VETA Mwanza)
aliyebuni mashine ya kuzoa na kuchoma magugu maji.
Wakati huo huo, Adam Zacharia
Kinyekile wa Songwe naye amekuwa mshindi wa kwanza katika Kundi la Sekta Isiyo
Rasmi ambalo VETA pia iliratibu mchakato wa washiriki wa kundi hilo. Adam
amebuni mashine au chombo kinachoweza kutoa huduma mbalimbali za kiufundi,
uchakataji na usindikaji wa mazao pamoja na huduma zingine mashambani.
Aliyefuatia katika
kundi hilo ni Abdul Lwangisa kutoka Gongo la Mboto, Dar es Salaam aliyebuni
mashine ya kuchakata takataka ngumu na kutengeneza vipuri vya mashine na vyombo
mbalimbali.
Wa tatu katika kundi
hilo ni Patrick Mpili akiwakilisha kampuni ya Giant of Genius ambao
wametengeneza ingine ya ndege (Jet Engine).
Makundi mengine
yaliyoshiriki mashindano hayo ni Kundi la Shule za Sekondari (lililoratibiwa na
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Ofisi ya
Rais-TAMISEMI); Kundi la Vyuo vya Ufundi Sanifu (lililoratibiwa na Taasisi ya
Teknolojia Dar es Salaam-DIT); Kundi la Vyuo Vikuu na Kundi la Taasisi za
Utafiti na Maendeleo (yaliyoratibiwa kwa pamoja na Tume ya Taifa ya Sayansi na
Teknolojia-COSTECH).
Akifunga mashindano
hayo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Prof. Joyce Ndalichako
aliwahimiza wabunifu kujikita zaidi katika kutafuta suluhu za changamoto
mbalimbali katika jamii.
Alisema vijana wengi
wanaosoma na kuhitimu mafunzo ya ufundi stadi wanaonesha kuwa mahiri na
wabunifu katika fani zao akitolea mfano wa baadhi ya vijana (waliohitimu VETA
Moshi) kwa kuonesha umahiri na kupata ithibati za kimataifa katika eneo la
uungaji vyuma.
Mafunzo yetu ya
ufundi stadi yako vizuri na ndio maana serikali imejikita katika kupanua fursa
za elimu na mafunzo ya ufundi stadi na tunaendelea na ujenzi wa vyuo vya mikoa
na wilaya.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi Mkuu wa VETA Daktari Pancras Bujulu aliwapongeza wabunifu na kusema
kuwa VETA ina dhamira ya kusaidia uendelezaji ubunifu katika eneo la ufundi
stadi.
Aliwahimiza wabunifu
kuendelea kutumia vipaji vyao kubuni vitu mbalimbali ili kutatua changamoto
mbalimbali katika jamii.
“Tumezoea kuagiza
vitu kutoka Ulaya, kumbe tunaweza kutengeneza vitu vingi hapahapa,” alisema.
Alisema mchakato wa
mashindano ya ubunifu mwaka huu utasaidia zaidi kuwafahamu wabunifu mbalimbali
na kuona ni namna gani ya kuwaendeleza na kuwasaidia katika ubunifu wao.
No comments:
Post a Comment