Mamlaka ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imesaini makubaliano ya ushirikiano na Taasisi
ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kwa lengo kuu la kuboresha utoaji mafunzo
katika sekta ya ngozi ili kuchangia kukuza sekta hiyo nchini na kusaidia juhudi za kuelekea kwenye uchumi wa viwanda.
Akizungumza wakati wa
tukio la utiaji saini makubaliano hayo Aprili 24, 2019 katika Taasisi ya DIT Dar es Salaam, Mkuu wa
DIT Profesa Preksedia Ndomba amesema makubaliano hayo yanalenga kupanua wigo wa
utoaji mafunzo na kuimarisha mafunzo ya ufundi na kuzalisha nguvu kazi mahiri
ya kuhudumia sekta ya ngozi kupitia mradi unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Alisema DIT inalenga
kutumia baadhi ya programu zinazotolewa katika vyuo vya VETA ili kupata vijana
walioiva katika fani mbalimbali watakaojiunga kwenye programu zinazotolewa na
Taasisi hiyo katika ngazi ya ufundi Sanifu.
Profesa Ndomba alisema
kupitia makubaliano hayo taasisi hizo zitaanza utekelezaji wa utoaji na
uboreshaji wa mafunzo hayo katika vyuo vya DIT- Kampasi la Mwanza, Chuo cha
VETA Dakawa na Chuo cha VETA Dodoma ikiwa ni pamoja na kuboresha karakana na
kuweka vifaa vya kisasa vya utoaji mafunzo hayo.
Alisema kwa sasa
DIT–Kampasi ya Mwanza inafanya usajili wa kutoa mafunzo ya ngazi ya tatu ya
ufundi ili kuwezesha vijana wanaohitimu katika chuo cha VETA Dakawa kwa ngazi
ya pili ya ufundi stadi kujiunga na chuo cha DIT Mwanza na kuendelea hadi ngazi
ya Ufundi Sanifu.
“Tunaamini kupitia
ushirikiano huu tutaweza kuongeza udahili katika chuo chetu cha Mwanza na
kuzalisha wataalamu zaidi watakaoweza kuitumikia sekta ya ngozi na walimu wa
kufundisha fani hii katika vyuo vya VETA.” Alisema
Mkurugenzi Mkuu wa VETA
Dkt. Pancras Bujulu amesema ushirikiano huo utaisaidia VETA kuongeza uzalishaji
wa mafundi stadi kwa ajili ya viwanda vya ngozi na bidhaa zitokanazo za ngozi.
Alisema kwa sasa VETA
kupitia chuo chake cha VETA Dakawa inatoa mafunzo ya utengenezaji wa bidhaa za
ngozi katika ngazi ya kwanza na ya pili ya ufundi na kwamba kupitia ushirikiano
huo wahitimu wa chuo hicho wataweza kupata nafasi za kujiendeleza na mafunzo
kwa ngazi ya tatu kupitia DIT-Kampasi ya Mwanza.
Dkt Bujulu aliongeza kuwa
kupitia DIT, VETA itapata waalimu wa kufundisha fani hiyo mpaka ngazi ya tatu
katika chuo cha Dakawa na kuweza kupanua wigo wa utoaji mafunzo katika vyuo
vingine vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini, hasa maeneo ya wafugaji ili
kusaidia wafugaji kuongeza thamani ya
mifugo yao.
“kwa sasa tuna changamoto
ya wataalam pamoja na vifaa vya kufundisha fani hii katika vyuo vyetu na ndiyo
maana hatujaweza kutoa mafunzo hayo hadi ngazi ya tatu ya ufundi….kupitia
ushirikiano huu tunaamini changamoto hii itapata ufumbuzi.” Alisema
Alisema pia VETA
itaanzisha mafunzo ya usindikaji na uchakataji ngozi katika chuo cha VETA
Dodoma ambacho kwa sasa kinaendesha fani ya Usindikaji Nyama ili kujihakikishia
upatikanaji wa malighafi bora ya ngozi itakayotumika katika uzalishaji wa
bidhaa za ngozi.
No comments:
Post a Comment