Mkurugenzi Mkuu wa
Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), Pius Maneno
amewakumbusha Wahasibu kuzingatia maslahi ya umma kwani ndio matakwa ya msingi
ya taaluma ya Uhasibu.
Akifungua mafunzo ya
Viwango vya Kimataifa vya Uandaaji wa Mahesabu ya Sekta za Umma (International
Public Sector Accounting Standards) kwa watumishi wa Mamlaka ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kwenye Chuo cha VETA Dodoma, leo tarehe 20 Mei,
2019, Maneno alisema tofauti na baadhi ya taaluma ambazo wakati mwingine
mhusika hutazama maslahi binafsi, taaluma ya Uhasibu daima ni ya kuzingatia
maslahi ya umma.
“ndio maana hata
kaulimbiu ya Bodi yetu ni Msemakweli. Sisi si watu wa kupindisha pindisha kwa
maslahi ya mtu binafsi, mara zote tunazingatia maslahi ya umma na kusema
ukweli,” alisema.
Sambamba na hilo,
Maneno aliwaomba Wahasibu wa VETA kuhakikisha mahesabu ya taasisi yanapangwa
vyema kwa kuzingatia viwango vya uhasibu na kuialika VETA kuingia katika
mashindano ya Upangaji Bora wa Mahesabu ambayo NBAA imeyaanzisha.
“unaweza kupata hati
safi ya ukaguzi wa hesabu zako, lakini mahesabu yako yakawa hayajapangwa
vizuri, ndio maana NBAA tumeanzisha mashindano hayo na nawaomba VETA muingie
kwenye kinyang’anyiro hicho,” alisema.
Aliongeza kuwa NBAA
inafikiria kupunguza muda wa uandaaji na uwasilishaji wa taarifa za ukaguzi wa
hesabu, kwani muda wa miezi sita wa sasa ni mrefu mno na endapo kwenye taarifa
kuna dosari zinazohitaji marekebisho, mhusika anaweza asipate muda wa kutosha
kuzirekebisha kabla ya mwaka mpya wa fedha.
Akitoa neno, Kaimu
Mkurugenzi wa Fedha wa VETA, Anthony Kasore alisema VETA imekuwa ikizingatia
viwango, misingi na taratibu za uandaaji wa mahesabu na kwamba kumekuwa na
ushirikiano wa karibu miongoni mwa wahasibu kutoka kanda na vituo mbalimbali
vya VETA katika kuandaa mahesabu na kuhakikisha yanakaguliwa kwa wakati.
Alisema, ili
kuhakikisha kuwa wahasibu wa VETA wanaendelea kuongeza maarifa na kukidhi
viwango na vigezo vya taaluma, Mamlaka imekuwa ikiandaa mafunzo na semina
mbalimbali za kuwajengea uwezo na kuwaimarisha.
No comments:
Post a Comment