Mamlaka ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeingia
makubaliano na Shirika la Kimataifa la Swisscontact kwa lengo la
kuboresha mfumo wa upatikanaji wa taarifa za soko la ajira ili kuimarisha utoaji
mafunzo ya ufundi stadi.
Makubaliano ya mradi
huo uliopewa jina la Ujuzi kwa Ajili ya Ajira (Skills for Employment Tanzania)
yamesainiwa leo Mei 14, 2019 katika ofisi za VETA Makao Makuu kati ya
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, na Msimamizi wa Mradi wa Swisscontact,
Ndg. Soren Poulsen.
Akizungumza wakati wa
kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, amesema
mradi huo utasaidia kuongeza fursa za ajira kwa vijana wanaohitimu mafunzo ya
Ufundi stadi kupitia upatikanaji wa taarifa sahihi za mahitaji ya soko
zitakazosaidia kuhuisha mitaala ya utoaji mafunzo.
“Tunatambua umuhimu
wa taarifa za soko la ajira katika kuboresha utoaji mafunzo na kuzalisha nguvu
kazi inayohitajika na soko la ajira ndiyo maana tunaona kuwa mradi huu utakuwa
wa manufaa kwetu.” Alisema
Naye Msimamizi wa
Mradi wa Swisscontact Ndg. Soren Poulsen, alisema kuwa anaamini kuwa mradi huo
utatoa mchango mkubwa katika kuboresha mchakato wa ukusanyaji taarifa za soko
la ajira na kuimarisha mahusiano kati ya watoa mafunzo na waajiri nchini.
Alitaja maeneo ambayo
yatapewa kipaumbele kupitia mradi huo kuwa ni pamoja na kuwajengea uwezo
wakusanya taarifa wa Mamlaka (Labour Market Analysts), kuboresha mbinu za
ukusanyaji taarifa, kuongeza ushiriki wa waajiri katika utoaji taarifa za
mahitaji yao ili kusaidia ukuzaji wa mitaala na kukiongezea uwezo Chuo cha
Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC) katika utoaji na usimamizi wa mafunzo.
Makubaliano hayo
yatadumu kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2019 hadi 2022 na muda utaweza
kuongezeka kulingana na makubaliano ya pande zote mbili.
No comments:
Post a Comment