Mamlaka
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri
Mkuu – Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu
imewajengea uwezo watahini 256 kwa ajili ya kuendesha awamu ya pili ya zoezi
la kurasimisha ujuzi kwa mafundi 10,443 nchini.
Akizungumza
wakati wa kufunga semina kwa watahini hao kwenye chuo cha VETA Singida Julai
17, 2019, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA Anthony Kasore alisema kuwa semina hiyo
ililenga kutoa mfunzo ya kuwawezesha watahini hao kuendesha zoezi la tathmini
kwa ufanisi.
Semina
hiyo iliyojumuisha watahini kutoka katika vyuo vya Ufundi Stadi na kutoka
viwanda mbalimbali ilifanyika katika chuo cha VETA Singida tarehe 8 hadi 17 Julai
2019.
Kasore aliwataka watahini
kufuata miongozo na maelekezo waliyopewa juu ya uendeshaji wa zoezi hilo na
kuwataka kutanguliza uzalendo na uadilifu katika hatua zote za utekelezaji wa
kazi hiyo.
“Nawaomba sana mzingatie
taratibu zote zinazotakiwa katika utekelezaji wa zoezi hili,” alisema
Kwa
mujibu wa Kasore, zoezi hilo la tathmini linatarajiwa kuanza Julai 30, 2019
nchi nzima ambapo mafundi
waliopata ujuzi kupitia mfumo usio rasmi watafanyiwa tathmini kulingana na ujuzi walionao kisha kupewa
mafunzo kuziba mapungufu na hatimaye kutunukiwa vyeti ambavyo vitawawezesha
kutambulika na kukubalika katika mfumo rasmi wa ajira.
Alisema katika
awamu ya kwanza jumla ya vijana 3,989 wanaume 3,539 na wanawake 450
walirasimishwa ujuzi wao.
Naye Mratibu wa programu hiyo kutoka VETA, Bwire Ally
alisema kuwa katika mafunzo hayo watahini hao walifundishwa namna ya kutambua,
kukusanya takwimu na kufanya tathmini ya ujuzi kwa mafundi.
Bwire alisema kukamilika kwa mafunzo hayo kumeongeza
idadi ya watahini kutoka 344 hadi 600 ambao watafanya tathmini katika maeneo
mbalimbali nchini.
Alisema
miongoni mwa faida za programu hiyo ni
kuwasaidia mafundi waliojifunza kupitia sehemu za kazi (wanagenzi) kupata kazi
zenye staha; kuwawezesha kushiriki na kushindana kikamilifu katika soko la
ajira; pamoja na kuinua tija mahali pa kazi na kusaidia waajiri wenye makampuni
kukidhi viwango katika eneo la rasilimali watu.
Mmoja wa
watahini waliopatiwa mafunzo hayo kutoka chuo cha VETA Iringa Gereon Mmole
alisema kuwa mafunzo hayo yamewaongezea mwanga zaidi na uelewa juu kuendesha
zoezi la tathmini kwa mafundi.
Zoezi la
utambuzi na urasimishaji wa ujuzi (Recognition of Prior Learning – RPL) linaloendeshwa
na VETA kwa kushirikiana na ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na wenye
Ulemavu lilianza
Julai 3, 2017 ambapo
katika awamu ya kwanza jumla ya vijana
3,989 wanaume 3,539 na wanawake 450 walirasimishwa ujuzi wao.
No comments:
Post a Comment