Wizara
ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeahidi kusaidia ubunifu wa “Pikipiki Salama”
uliofanywa na Mwalimu wa Chuo cha VETA Kipawa, Aneth Mgana ili kuwezesha
kuingia katika matumizi.
Ahadi
hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja
Jenerali Jacob Kingu alipotembelea chuo cha VETA Kipawa Alhamisi, tarehe 18
Julai 2019 ili kujifunza zaidi juu ya ubunifu huo.
Meja
Jenerali Kingu ameipongeza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)
kwa ubunifu huo akisema kuwa utasaidia kwa kiasi kikubwa kulinda usalama wa
dereva, abiria na watumiaji wengine wa pikipiki ambao wamekuwa wakiathiriwa kwa
kiasi kikubwa na ajali za pikipiki.
Alisema
Wizara yake ipo tayari kuuwezesha ubunifu huo kuingia katika matumizi na
kumtaka mbunifu wa pikipiki hiyo Aneth Mganga kuainisha na kuwasilisha mahitaji
yake Wizarani.
Ubunifu
uliopo kwenye “Pikipiki Salama” ni wa mfumo unaozuia pikipiki kuwaka endapo
dereva hajavaa kofia ngumu (helmet).
Mbunifu
pia anapanga kuongeza kipengele cha kuzuia pikipiki kuwaka endapo dereva
amelewa pombe, kutoa taarifa endapo dereva amebeba abiria anayetaka kumdhuru na
kutoruhusu kubeba abiria zaidi ya uwezo wake, maarufu kama mshikaki.
Aidha
Katibu Mkuu huyo alisema kuwa Wizara yake itaishirikisha VETA kwenye mpango wa
kuandaa tela maalum itakayofungwa kwenye pikipiki kwa lengo la kusaidia
kuepusha ajali na kuongeza kipato kwa waendesha bodaboda.
“Tunahitaji
sana utaalamu wa watu wa VETA katika mradi huu tunaoufanya hasa upande wa
TEHAMA na hivyo tutahakikisha mnashiriki kikamilifu ili kwa pamoja tuweze
kuondoa wimbi la ajali za pikipiki” Alisema
Taasisi
zingine zinazohusika kwenye mradi huo ni Shirika la Mzinga, Shirika la Nyumbu,
Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO)
na Chuo cha Usafirishaji nchini (NIT).
Katika
ziara hiyo, Katibu Mkuu aliongozana na Wajumbe wa Kamati Maalum ya Wataalam ya
Udhibiti wa ajali za pikipiki ambao nao walitoa mawazo yao katika kuiboresha
pikipiki hiyo ili iweze kuendana na mazingira halisi ya hapa nchini.
Takwimu
zinaonyesha kuwa kwa miaka kumi (2009 – 2018) jumla ya watu 35,231 wamejeruhiwa
kufuatia ajali za pikipiki huku vifo vilivyotokana na ajali hizo vikiwa ni
8,004.
No comments:
Post a Comment