CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Monday, 2 December 2019

DC awataka wahitimu wa VETA kuleta mapinduzi kwenye kilimo



Mkuu wa Wilaya ya Babati mkoani Manyara, Elizabeth Kitundu amewataka wahitimu wa mafunzo ya ufundi stadi kutumia vyema ujuzi walioupata kuboresha sekta ya kilimo.

Akizungumza wakati wa mahafali ya sita ya Chuo cha VETA Manyara Novemba 14, 2019 Kitundu alisema kupitia mafunzo ya zana za kilimo na utengenezaji wa mitambo ya kilimo wahitimu katika fani hizo wana fursa ya kufanya mapinduzi ya kilimo katika mkoa huo.

Aliwataka wahitimu hao wa VETA kueneza ujuzi walioupata kwa wakulima ili waweze kutatua changamoto zinazowakabili katika kilimo na kuwatengenezea nyenzo rahisi za kuwarahisishia kilimo.

“Nina uhakika kabisa Kijana aliyesoma fani hii ya zana za kilimo, hawezi kukosa ajira hasa ukizingatia kuwa Wilaya ya Babati na Mkoa wa Manyara kwa ujumla umetawaliwa na shughuli za kilimo … matrekta yako mengi yanalima huko vijijini, pikipiki na bajaji ziko nyingi, lazima watahitajika mafundi wa kutengeneza na kuziendesha,” alisema

Kuhusu wanafunzi wanaosomea ufundi wa magari, alisema wana uwezo wa kufungua karakana za kutengeneza magari kwa kuanzia na vifaa vichache ambavyo gharama zake ni nafuu.

Kitundu alisisitiza nidhamu na uaminifu katika kazi  kwa vijana hao na kwamba mambo hayo yatawawezesha kuendeleza biashara zao na kutoa ajira kwa vijana wengine.

Aliwashauri viongozi mbalimbali wa halmashauri ya wilaya na mji kupeleka vijana kwa makundi kupata mafunzo ya ufundi kwenye fani mbalimbali na ujasiriamali yatakayowezesha kukuza uchumi wa Mkoa huo.

Mkuu wa chuo cha VETA Manyara Felix ole Ndukai alisema jumla ya vijana 188 wamehitimu mafunzo kwa daraja la pili katika fani za Uhazili, Uungaji vyuma, useremala, uashi, ufundi wa zana na mitambo ya kilimo, umeme, maabara, Ufundi magari na Elektroniki.

Alitaja baadhi ya changamoto zinazokabili chuo hicho kuwa ni upungufu wa mabweni, upungufu wa karakana na madarasa na uhaba wa nafasi za mafunzo kwa vitendo viwandani.



No comments:

Post a Comment