Wahitimu
wa VETA wasisitizwa kutumia TEHAMA kujiajiri
Mkurugenzi Mkuu wa Tume
ya Taifa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) Mhandisi Samson Mwela
amewataka wahitimu wa VETA kuitumia vyema taaluma ya Tehama kujiajiri.
Akizungumza katika Mahafali
ya Chuo cha VETA Kipawa Novemba 22,2019. Mhandisi Mwela amesema kuwa Serikali
imewekeza sana katika miundombinu ya Tehama ambapo asilimia 94 ya maeneo
yanayokaliwa na watu yamefikiwa na miundombinu ya mawasiliano.
Amesema kuwa vijana
waliohitimu katika Chuo hicho ambacho kinaendesha kozi ya Tehama wana fursa za
kujiajiri kutokana na Mazingira wezeshi ya Serikali katika miundombinu.
Amewataka vijana
kuchangamkia fursa hizo hasa kwa kuzingatia kuwa fursa kwenye sekta hiyo
hazihitaji mtaji mkubwa kuweza kujiajiri na kuwasisitiza kuwa waadilifu katika
kazi zao ili kuepuka Uhalifu kwa kutumia Tehama.
Naye Kamanda wa Polisi
Kikosi cha Usalama Barabani nchini Fortunatus Muslim alisema maendeleo ya
Tehama duniani yanagusa kila sekta na kwamba wahitimu hao wanaweza kutumia
fursa hiyo kutengeneza mifumo mbalimbali ya kurahisisha uendeshaji wa shughuli
mbalimbali.
Aliwakaribisha
wanafunzi kutembelea Jeshi la Polisi na kujionea mifumo mbalimbali inayotumiwa
na jeshi hilo na namna mifumo hiyo ilivyorahisisha uendeshaji wa shughuli
mbalimbali.
Mkuu wa Chuo cha VETA
Kipawa Dickson Mkasanga amesema kuwa Chuo hicho kinaendelea kufanya tafiti na
bunifu mbalimbali zinazolenga kutatua changamoto zinazoikabili jamii pamoja na
kuchangia katika uchumi wa viwanda.
Amesema jumla ya vijana
122 wamehitimu mafunzo chuoni hapo katika fani za Tehama, Elektroniki na
Kompyuta kwa ngazi za Ufundi Stadi Daraja la pili, Daraja la Tatu, Stashahada
pamoja na kozi za muda mfupi huku chuo hicho kikiwa na uwezo wa kudahili
wanafunzi 250 wa kozi ndefu na 1,800 wa kozi fupi kwa mwaka.
No comments:
Post a Comment