Mradi
huo unahusisha utoaji mafunzo katika fani ya Ufundi wa Zana za Kilimo (Agro-Mechanics)
katika chuo cha mafunzo ya ufundi na huduma cha Mkoa wa Manyara (Manyara RVTSC)
ulioanza mwezi Agosti, 2017 na unatarajiwa kumalizika Machi, 2020. Kiongozi
wa Timu kutoka Ujerumani inayofuatilia na kutathmini mradi huo Herman Roder
alisema kuwa mradi huo umefanikisha kutoa matokeo yaliyotarajiwa. Bwana Roder
alibainisha kuwa timu hiyo imeridhishwa na hatua zilizofikiwa katika kutekeleza
mradi huo ambapo masuala yaliyozingatiwa katika tathmini ni pamoja na Umuhimu
wa mradi (relevance), Ufanisi katika utekelezaji (effectiveness), Upatikanaji
wa matokeo tarajiwa (efficiency) na Uendelevu wa mradi (sustainability).
Maelezo
hayo yalitolewa wakati Timu hiyo ilipokutana na Uongozi wa VETA wakati wa kupokea
mrejesho wa Ufuatiliaji na Tathmini ya utekelezaji wa mradi huo katika ofisi za
VETA Makao Makuu, tarehe 4 Novemba, 2019.
Baada
ya kupokea taarifa hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu alisema
kuwa VETA itaendelea kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mradi huo, kwani
unatoa mafunzo mahali pa kazi na hivyo kuandaa nguvukazi yenye kukidhi mahitaji
ya soko la ajira.
Dkt. Bujulu aliwahakikishia wajumbe wa Timu hiyo kuwa VETA
itafanya jitihada za kueneza utaratibu wa mafunzo ya Uanagenzi wa Zana za Kilimo katika
vyuo vingine vya Ufundi Stadi vya Arusha, Kihonda, Dakawa na Mpanda.
Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Mhe. Jitu Son, alishiriki
katika kikao hicho ambapo alikiri kuwa mfumo wa mafunzo ya uanagenzi umekuwa wa
manufaa kwa wananchi wa Jimbo lake na Mkoa wa Manyara kwa ujumla. Mhe. Jitu Son
aliishauri VETA kushirikisha wadau wengi zaidi ili utaalam wa utunzaji na
matumizi ya zana za kilimo uweze kuenea kwa wakulima wengi zaidi na kuongeza
tija katika Sekta ya Kilimo.
Timu
hiyo pia ilibainisha utayari wa kuendelea na awamu ya pili ya mradi huo kwa
miaka mitatu kuanzia Aprili, 2020 huku ikifurahishwa na ushirikiano unaotolewa na
VETA katika utekelezaji wa mradi huo, ikiwa ni pamoja na utayari wa kugharamia
baadhi ya shughuli za mradi.
Mafanikio
yaliyotokana na utekelezaji wa mradi huo ni pamoja na mafunzo kwa walimu na
wakulima, ambapo jumla ya walimu 25 na wakulima 15 walipatiwa mafunzo katika
kozi za uchomeleaji na uungaji vyuma na mbinu za ufundishaji kozi za Kilimo. Walimu
hao walitoka katika vyuo vya VETA Songea, VETA Mpanda, VETA Dar es Salaam, VETA
Arusha, VETA Kihonda, VETA Manyara na Chuo cha Ufundi Stadi Kilacha. Vilevile,
kupitia mradi huo jumla ya wanagenzi 26 walidahiliwa mwezi Februari, 2019 na wanaendelea
na mafunzo katika fani ya Ufundi wa Zana za Kilimo.
Pamoja na mafunzo ya Uanagenzi, wananchi wa Babati Vijijini wamepata fursa za kujifunza juu ya matumizi na utunzaji wa zana ya kilimo pamoja na mbinu za kuzuia upotevu wa mazao baada ya mavuno (Prevention of Post-harvest Losses).
Pamoja na mafunzo ya Uanagenzi, wananchi wa Babati Vijijini wamepata fursa za kujifunza juu ya matumizi na utunzaji wa zana ya kilimo pamoja na mbinu za kuzuia upotevu wa mazao baada ya mavuno (Prevention of Post-harvest Losses).
Mfumo wa utoaji mafunzo ya Uanagenzi unahusisha kuhudhuria mafunzo
ya darasani (VETA) na kufanya vitendo katika viwanda na mashamba au sehemu
nyingine za kazi. Mafunzo hayo ni ya miaka mitatu ambapo kwa kila mwaka
mwanagenzi anatumia wiki 20 kwa mafunzo ya darasani na wiki 32 kwa mafunzo ya
viwandani.
No comments:
Post a Comment