Wananchi wa Wilaya ya Wanging'ombe mkoani Njombe wanatarajia kuanza kupata mafunzo ya ufundi stadi katika Chuo cha VETA kinachotarajiwa kuanzishwa Wilayani Wanging'ombe katika mwaka wa masomo ujao.
Hayo yamebainishwa
tarehe 4 Agosti, 2021 na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu,
alipotembelea na kukagua majengo na miundombinu katika Kijiji cha Ufwala,
ambayo itakarabatiwa na kuboreshwa ili
kukidhi mahitaji ya msingi ya chuo cha ufundi stadi.
Dkt. Bujulu amesema
Chuo hicho kitaanzishwa katika majengo na miundombinu iliyokuwa ikimilikiwa na
Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe kufuatia Halmashauri hiyo kukabidhiwa na
Wakala wa Barabara nchini (TANROADS). Awali, majengo hayo yalitumiwa na
Mhandisi Mkazi aliyesimamia ujenzi wa
Barabara ya Nyigo-Igawa, mkoani Njombe.
Kwa mujibu wa Dkt.
Bujulu, Halmashauri ya Wilaya ya Wanging'ombe ilikabidhi majengo hayo kwa VETA
mwezi Mei, 2020 baada ya wananchi wa Wilaya hiyo kupendekeza majengo hayo
yatumike kutoa mafunzo ya ufundi stadi.
Mwenyekiti wa Kijiji
cha Ufwala kilipo Chuo hicho, Bw. Failos Ng'umbi, amesema kuwa wananchi wa
kijiji chake wanasubiri kwa hamu kubwa kuanza kwa mafunzo Chuoni hapo.
Alisema mahitaji ni
makubwa mno Wilayani humo, hivyo akaiomba VETA kuharakisha matayarisho, ili
mafunzo hayo yaweze kuanza haraka iwezekanavyo. Mwenyekiti huyo amebainisha
kuwa kijiji chake kiko tayari kutoa ardhi ya nyongeza kwa kadri ya mahitaji ya
VETA kwa ajili ya kupanua Chuo hicho. Kwa niaba ya Mamlaka, Mkurugenzi Mkuu
alimshukuru Mwenyekiti na viongozi wengine waliohudhuria ukaguzi huo, wakiwemo
Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Wanging’ombe Bw. Erasto Danda, Ofisa Mtendaji wa
Kata ya Wanging’ombe (WEO) Bi. Beth Mangula na Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha
Ufwala (VEO) Bi. Irene Nungwi.
No comments:
Post a Comment